Rais wa Marekani, Donald Trump ametangaza kusitisha mara moja safari za ndege za Boeing chapa 737 MAX 8, baada ya ndege kama hiyo ya Ethiopia kuanguka Jumapili iliyopita na kusababisha vifo vya watu wote 157 waliokuwemo ndani ya Ndege hiyo.
Akizungumza na waandishi habari katika Ikulu ya Marekani, Trump amesema amezipiga marufuku ndege hizo kuruka kutokana na kuongezeka kwa shinikizo la kimataifa na kisiasa, lililokuwa likiitaka Marekani kufuata nyayo za nchi nyingine kadhaa duniani kuzipiga marufuku ndege hizo kuruka katika anga yake.
Aidha, baada ya tangazo hilo la Trump, Shirika la Mamlaka ya Anga la Marekani, FAA lilisitisha mara moja kurusha ndege hizo, huku Trump akisema kuwa ndege ambazo ziko safarini, zitazuiwa mara baada ya kutua.
Hata hivyo, Ajali ya Ethiopia imetokea miezi mitano baada ya ndege ya aina hiyo ya shirika la ndege la Indonesia, Lion Air kuanguka baharini na kusababisha vifo vya watu 189. ambapo Trump amesema ana matumaini kampuni ya kutengeneza ndege nchini Marekani, Boeing itatoa majibu sahihi kutokana na ajali hiyo.