Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM) wilayani ya Rorya mkoani Mara, Charles Ochele amewahimiza vijana kujiunga na vikundi ili waweze kupata mikopo isiyo na riba itakayowasaidia katika shughuli zao za kimaendeleo ikiwemo miradi ili kujikwamua kimaisha.
Ameyasema hayo kwenye kikao cha Baraza la Umoja wa Vijana (UVCCM) wilaya humo kilichokuwa kikijadili na kupokea taarifa ya mpango kazi, mikakati kutoka kila Kata kwa mwaka 2019, kupokea taarifa ya Mpango kazi na mikakati kutoka ofisi ya Vijana Wilaya na maelekezo mbalimbali.
Amesema kuwa mikopo ya sasa haina riba lakini anasikitika kuwa Vijana wa CCM hawajitokezi kuanzisha vikundi vya miradi, ili halmashauri ya Wilaya iwapatie mikopo inayotokana na vyanzo vya ndani asilimia kumi ya makusanyo yake kati ya hizo asilimia 4 ni kwa Wanawake,4 Vijana na 2 Walemavu, huku akiwahimiza kujitokeza wanufaike na mikopo hiyo.
”Ugomvi wangu mkubwa kwenye Halmashauri ulikuwa ni hii asilimia kumi ambayo ilikuwa haitolewi inavyotakiwa, nashukuru kuona Afisa wa Idara ya Maendeleo ya Jamii kaja kuwapa elimu Vijana namna ya kuanzisha vikundi na kukopa hivyo ni matarajio yangu elimu mliyoipata itawasaidia na mtaanzisha vikundi vingi,”amesema Ochele.
Akitoa elimu juu ya vigezo vya kuanzisha vikundi na Mikopo, Kaimu Afisa Maendeleo ya Jamii Halmashauri ya wilaya hiyo, Majura Mgeta amesema kuwa kuna vikundi 985 vilivyosajiliwa vikiwemo vya Wanawake, Vijana na Walemavu.
Aidha, Mgeta alizitaja sifa za kuanzisha kikundi kwa upande wa Vijana ni kuanzia mtu mwenye umri wa miaka 15-35, kikundi kiwe na nia moja na malengo, kiwe na watu 5 na kuendelea ,Katiba, Usajili wa kikundi, Akaunti, shughuli wanazofanya na kwamba ili ukope kikundi kiwe kinakopesheka.
Kwa upande wake, George Peter mkazi wa Kijiji cha Ralanya amesema kuwa sababu ya Vijana kutojitokeza kukopa ni kutopata taarifa kwa wakati za matangazo ya mikopo na wengine kutofahamu sifa za kuanzisha vikundi na kwamba elimu waliyoipata imewasaidia na kuahidi kujiunga na vikundi kufanya shughuli za miradi zitakazo wawezesha kukopa na kurejesha mkopo kwa wakati.