Watu wanaosadikika kuwa ni abiria wa daladala, maarufu kama ‘matatu’ nchini Kenya, wamempiga dereva wa chombo hicho cha usafiri kwa madai kuwa uendeshaji wake haujali uhai wa abiria.
Video ya tukio hilo imesambaa kwenye mitandao ya kijamii hususan mtandao wa Twitter ambao ni maarufu zaidi nchini humo.
Matatu hiyo inamilikiwa na Lina Sacco ikiwa na nambari za usajili, KCL 740B, imeripotiwa kuwa ilikuwa ikitoka Limuru kuelekea Nairobi.
Abiria hao wameeleza kuchukizwa na tabia ya dereva huyo pamoja na rafiki yake walipokuwa barabarani na kwamba walionekana kutojali kabisa maisha yao.
Mmoja kati ya abiria alisikika akisema, “tumemkataza kukimbia, anataka kutuua kwa nini?”
Hivi karibuni kumekuwa na ripoti ya matukio mengi ya ajali za barabarani jijini Nairobi, hali ambayo imewafanya abiria kutowaamini madereva.
Kupitia mitandao ya kijamii, wengi wameonesha kuunga mkono kitendo cha abiria hao.
Jeshi la polisi jijini Nairobi limeeleza kuwa linafanya uchunguzi wa tukio hilo kwa kuanzia kwenye video iliyosambaa, huku ikionya wananchi kutojichukulia sheria mikononi.