Serikali ya Nepal imefungia mchezo maarufu wa video (video game) unaochezwa mtandaoni, unaofahamika kama PlayerUnknown’s Battlegrounds (PUBG), baada ya kukubaliana na wazazi kuwa mchezo huo unawaathiri watoto kisaikolojia.
Leo, Mamlaka ya Mawasiliano nchini humo imewaagiza watoa huduma ya internet wote kuufungia mchezo huo na kutouonesha kwa namna yoyote.
Wazazi nchini humo walifungua kesi mahakamani pamoja na kukusanya sahihi kadhaa kuomba mchezo huo ufungiwe.
“Mahakama iliamuru Polisi kufanya uchunguzi na kuwashirikisha wataalam wa masuala ya kisaikolojia, baada ya muda ilibainika kuwa madai ya wazazi hao yana ukweli. Hivyo, ili kuwalinda watoto na vijana wenye umri mdogo Serikali imeufungia mchezo huo,” Msemaji wa Mamlaka ya Mawasiliano ya Nepal, Sandip Adhikari ameliambia sherika la habari la Ujerumani la DPA.
India pia imeufungia mchezo huo, hasa baada ya kuripotiwa kuwa kijana mmoja mdogo alijiua akipinga wazazi wake kujaribu kumzuia asiucheze. Waziri wa jimbo la Goa ameutaja mchezo huo kama ‘shetani wa kila nyumba’.
Mchezo huo unachezwa kwenye simu janja, ipad na kompyuta, ni kati ya michezo yenye mauzo makubwa zaidi ukiwa na wachezaji takribani milioni 400 kwa ujumla.