Mamlaka ya Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA) imeikabidhi Serikali mradi wa ujenzi wa Zahanati uliojengwa kwa ushirikiano kati ya TANAPA, Halmashauri ya Wilaya ya Muleba na Wananchi wa Kijiji cha Ikuza kilichopo Kisiwani Ikuza ambapo mradi huo umegharimu kiasi cha shilingi milioni 280,953,625/= hadi kukamilika kwa hatua ya kwanza ya ujenzi wa vyumba kumi na moja vya vyakutolea huduma.
 
Akikabidhi Zahati hiyo, Naibu Kamishina Mkuu wa TANAPA, Martin Leboki aliyemwakilisha Mkurugenzi Mkuu TANAPA Taifa. Alani Kijazi amemweleza Mkuu wa Mkoa wa Kagera na wananchi waliohudhuria hafla fupi ya makabidhiano kuwa zahanati hiyo imejengwa na kukamilika kwa ushirikiano mkubwa kati ya Halmashauri ya Wilaya ya Muleba na wananchi wa kijiji cha Ikuza kutokana na ujirani mwema wa Hifadhi ya Taifa ya Rubondo.
 
Amesema kuwa TANAPA ilitoa jumla ya shilingi milioni 144,725,675/= katika ujenzi wa zahanati hiyo yenye vyumba kumi na moja na kununua vifaa tiba kama vitanda vya wagonjwa, vitanda vya akinamama wajawazito kujifungulia pamoja na samani nyingine zitakazotumika katika zahanati hiyo, ambapo Halmashauri ya Wilaya ya Muleba ilichangia jumla ya shilingi milioni 124,392,340/= na wananchi walichangia jumla ya shilingi milioni 14,535,000/=
 
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Kagera Brigedia Jenerali Marco E. Gaguti ameishukuru TANAPA kwa kushirikiana na wananchi wa Ikuza na kuwajengea Zahanati ya kuwahudumia na kuwaondolea changamoto ya upatikanaji wa huduma ya afya katika kisiwani humo pamoja na visiwa vya jirani.
 
Aidha, amesema kuwa pamoja na Serikali kuendelea kuboresha huduma za afya kwa kasi kubwa tangu mwaka 2015/16 lakini bado kuna uhitaji mkubwa hasa katika vijiji ambapo amesema kuwa mwaka 2015/16 mkoa wa Kagera ulikuwa unapokea fedha za afya shilingi milioni 800/= lakini hadi sasa mkoa unapokea shilingi bilioni 5 kwa mwaka, Wilaya ya Muleba ilikuwa inapokea shilingi milioni 400 lakini sasa inapokea shilingi bilioni 1 kwa mwaka.
 
Katika hatua nyingine Mkuu wa mkoa ametoa maagizo kuwa Zahanati hiyo inatakiwa kuanza kutoa huduma mara moja isikae tena mwaka bila kutoa huduma kwa wananchi.
 
Naye diwani wa Kata ya Ikuza, Fortunatus Wazia Matta ameishukuru TANAPA na Serikali kwa kuwasogezea karibu wananchi huduma ya afya kwani amesema kuwa tangu alipochaguliwa kuwa diwani wa kata ya Ikuza mwaka 2010 hadi sasa wakina mama wajawazito wanne tayari wamepoteza maisha yao kutokana na changamoto ya afya katika kata hiyo iliyopo visiwani.

Dkt. Bashiru azungumzia mjadala wa Katiba Mpya wa bungeni
Halmashauri Kuu CCM Taifa (NEC) yawapongeza viongozi mkoani wa Simiyu