Takribani watu 20 wameripotiwa kupoteza maisha na wengine 300 wamejeruhiwa baada ya mabomu kulipuka katika makanisa na hoteli kadhaa nchini Sri Lanka, Jumapili ya Pasaka.
Kwa mujibu wa vyombo vya habari vya nchini humo, mabomu yameripotiwa katika makanisa matatu ya Kochchikade, Katuwapitiya na Batticaloa ambayo yalikuwa yamelengwa na washambuliaji.
Aidha, hoteli za kitalii za hangri La, Cinnamon Grand na Kingsbury ambazo zote ziko katika jiji la Colombo nazo zilishambuliwa katika siku hii ya Pasaka ambayo husherehekewa kama kumbukumbu ya kufufuka kwa Yesu Kristo na watu wa imani ya Kikristo duniani kote.
Picha zilizosambazwa kwenye mitandao ya kijamii zimeonesha damu zilizomwagika ndani ya kanisa la Katuwapitiya, pamoja na hali ya taharuki iliyozuka kwenye makanisa mengine.
Polisi wamethibitisha kutokea kwa tukio hilo wakieleza kuwa wameanza kufanya uchunguzi wa haraka lakini pia wamefanikiwa kurejesha hali ya utulivu.
Afisa wa Hospitali ya Batticaloa ameiambia AFP kuwa wamewapokea majeruhi zaidi ya 300 kwenye hospitali hiyo ambao wamepata majeraha na mshtuko kutokana na milipuko hiyo. Polisi au Serikali bado haijataja idadi ya waliofariki, lakini vyombo vya habari vya kuaminika vimetaja idadi ya watu 20 huku wengine wakidai idadi imeongezeka hadi 49.