Leo Mei 3, 2019 Rais Magufuli katika uwekaji wa jiwe la msingi la ujenzi wa maktaba ya MUST Mbeya kwenye ziara yake amekemea sana vitendo vya ngono vyuoni na kuwataka wanafunzi kutochanganya masuala ya masomo na mapenzi.
Amesema hayo mara baada ya kukerwa na wanafunzi aliowaona wakikumbatiana chuoni hapo wakati akipita.
Magufuli amesema haiwezekani jamaa huyu akumbatie huku hajatoa mahari.
“Wakati nakuja nimemuona kijana amekumbatiana na kijamaa mmoja, nikasema angekuwa binti yangu, ningeteremka nimzabe kibao, wote wawili, haiwezekani akumbatiwe na jamaa ambaye hajatoa hata mahari… kukumbatiana kwanini ufanye barabarani? Kwanini usiende bwenini ukakumbatiane mpaka ulewe kukumbatiwa?.” amesema Magufuli.
Rais Magufuli amesema, vitendo vya kujihusisha na ngono vyuoni vinaathiri kwa kiasi kikubwa maendeleo ya elimu ya wanafunzi, na hata kusababisha serikali kutofikia malengo yake ya kuwa na vijana wasomi, kwa ajili ya kusukuma gurudumu la maendeleo ya taifa.
Aidha, amewataka wahadhiri wa vyuo kutowashawishi wanafunzi kufanya nao vitendo vya ngono, huku akiwataka baadhi yao wenye tabia ya kufelisha mitihani wanafunzi wanaowakataa kujihusisha nao kimapenzi, kuacha kabisa.