Idara ya Biashara ya Marekani, jana ilitangaza kuifungia kampuni kubwa ya China ya Huawei Technologies pamoja makampuni mengine 70 yanayoshirikiana na kampuni hiyo.
Hatua hiyo inapiga marufuku Huawei kutonunua vifaa vyovyote kwenye makampuni ya Marekani bila kupata kibali maalum cha Serikali, pamoja na kusambaza bidhaa zake mpya.
Maafisa wa Marekani wameiambia Reuters kuwa uamuzi huo unaiwekea ugumu kama sio kufanya iwe haiwezekani kabisa kwa Huawei ambayo ni kampuni kuwa zaidi duniani ya vifaa vya mawasiliano ya simu kuuza bidhaa zake kwenye soko la Marekani ambalo inalitegemea.
Kupitia katazo hilo ambalo linaanza kutumika siku chache zijazo, Huawei watalazimika kuwa na leseni maalum kwa ajili ya kuwaruhusu kununua vifaa au kutumia teknolojia yoyote ya Marekani.
Katibu wa Biashara, Wilbur Ross aemeeleza kupitia taarifa yake kwa vyombo vya habari kuwa Rais Donald Trump amebariki uamuzi huo ambao amedai utalinda teknolojia ya Marekani kutotumiwa na makampuni ya kigeni kwa hali ambayo itahatarisha usalama wa Marekani au sera za kigeni.
Idara ya Sheria ya Marekani ilieleza kuwa imebaini kuwa mwezi Januari mwaka huu, kampuni ya Huawei na makampuni mengine yalishirikiana kutoa huduma za kifedha kwa Iran kinyume na makatazo ya Marekani.
Idara hiyo ilihitimisha kuwa ina sababu za msingi zinazoonesha kuwa Huawei walijihusisha na shughuli ambazo ni kinyume na usalama wa Marekani au sera za nchi za nje.
Awali, Serikali ya Marekani inayoongozwa na Trump ilishawishi nchi nyingine kutotumia vifaa vya kampui ya Huawei kwa teknlojia ya kizazi kipya ya 5G.
Hivi karibuni, Serikali ya Marekani iliweka kodi mpya kwenye bidhaa za China hali iliyochagiza vita ya uchumi kati ya nchi hizo zenye nguvu kubwa duniani.