Nchini Kenya, Mahakama ya mji wa Eldoret imepata mshtuko mkubwa mara baada ya kubaini kuwa mtuhumiwa aliyekuwa akishikiliwa kwenye gereza la wanawake kwa kosa la udanganyifu ni mwanaume.
Mshukiwa huyo jina lake halisi ni Shieys Chepkosgei na kudanganya kuwa ni mwanamke na kutumia jina la Pamela Mulipi.
Siku ya Jumatatu alikamatwa katika Chuo na Hospitali ya Rufaa ya Moi ambapo alikua akifanya kazi kama muuguzi mwanafunzi wa kike ingawa hakusajiliwa hapo.
Na kosa hilo alilifanya mnamo June, 14 mwaka huu.
Baada ya kushtakiwa, alipelekwa kwenye gereza la wanawake la Eldoret kusubiri maamuzi ya mahakama huku akitambuliwa kama mwanamke ambapo siku ya Jumanne askari magereza katika ukaguzi wao wa kawaida waligundua kuwa mshukiwa huyo alikua mwanaume.
Hakimu wa mahakama hiyo Charles Obulutsa siku ya Jumanne alilazimika kutoa amri nyingine ikielekeza kuwa mshukiwa ashikiliwe kwenye kituo cha polisi cha Eldoret Magharibi ili kutoa nafasi ya kufanyika uchunguzi wa kitabibu kuthibitisha jinsia yake.
Taarifa hiyo imeripotiwa na Gazeti la Daily Nation la Kenya.
Awali, Hakimu Obulutsa aliamuru mtuhumiwa ashikiliwe gerezani mpaka tarehe 24 mwezi Juni, Gazeti la Daily Nation limeripoti.
Shauri hilo litatajwa tena tarehe 27 mwezi Juni.