Utafiti uliofanywa na Shule ya Tiba ya Chuo Kikuu cha Nottingham kimebaini kuwa unywaji wa kahawa mbali na kumfanya binadamu ‘aamke’, unaweza kusababisha kupungua uzito.
Profesa Michael Symonds ambaye aliongoza utafiti huo ameeleza kuwa kahawa husaidia kuhuisha uzalishaji wa mafuta ya mwilini yanayojulikana kama ‘brown fat’.
“Brown fat hufanya kazi tofauti kabisa na mafuta mengine mwilini na huzalisha mwili kwa kuchoma sukari na mafuta, hasa ikishindana na baridi,” alisema Profesa Symonds.
“Kazi yake inapozidi kufanyika inaongeza uwezo wa kudhibiti sukari mwilini na kuchoma ‘calories’ na matokeo yake husaidia katika kupunguza uzito,” aliongeza.
Kwa mujibu wa Jarida la Scientific Report, utafiti huo umekuwa wa kipekee ukiwa na matokeo ya kusaidia binadamu kupunguza uzito na kwamba utaleta mabadiliko ya kiafya katika jamii ambayo uzito uliopita kiasi umekuwa tatizo kwa wengi.