Mchezaji wa Senegal Krepin Diatta, ambaye alifunga goli la pili la Senegal kwenye mchezo wa kwanza wa AFCON dhidi ya Tanzania, amekaribishwa kuja kutalii nchini na Waziri wa Maliasili na Utalii, Dkt. Hamisi Kigwangalla.
Waziri Kigwangalla amemkaribisha mchezaji huyo, Krepin Diatta, kuja Tanzania kutembelea vivutio vya utalii vilivyopo nchini na serikali itagharamia gharama.
“Nitumie nafasi hii kukukaribisha Krepin Diatta kuja Tanzania kutalii katika Hifadhi ya Taifa ya Serengeti ambayo imetoka kutuzwa kuwa bora zaidi barani Afrika na Pori la Akiba kubwa zaidi Afrika, Selous. Tutagharamia safari yako hiyo,” aliandika Kigwangalla kupitia Instagram.
Aidha, Diatta alitawala katika mitandao ya kijamii hapa nchini baada ya kuifungia Senegal goli la pili katika mechi hiyo wiki iliyopita. “Waafrika wote ni ndugu na hata hii mipaka tunayoiona iliwekwa na wakoloni waliotutawala”, ameongeza Waziri.
Hata hivyo, Diatta anachezea klabu ya Brugge ya Ubelgiji anakocheza nahodha wa Taifa Stars, Mbwana Samatta, alieleza kusikitishwa na picha zake kusambaa mitandaoni kwa lengo la kumdharirisha.