Kampuni ya kutengeneza ndege ya Boeing imetangaza kwamba itatoa dola milioni mia moja kwa familia, serikali na mashirika yasiyo ya kiserikali ya Ethiopia na Indonesia, ili kusaidia familia na jamii za watu waliopoteza maisha yao kwenye ajali mbili za ndege muundo wa 737 MAX.
Kwa mujibu wa shirika la habari la Reuters, hatua hiyo ni katika juhudi za kuimarisha taswira ya kampuni hiyo ambayo hadhi yake imeshuka kwa kiwango kikubwa katika siku za karibuni,
Aidha, hii ni kufuatia ajali ya mwezi Machi mwaka huu iliyozua utata, ambapo abiria wote 157 wa ndege ya shirika la Ethiopia Airlines waliokuwa safarini kutoka Addis Ababa, Ethiopia, kuelekea Nairobi nchini Kenya na ile ya ndege ya shirika la Indonesia Airlines iliyotokea mwaka 2018.
Mkurugenzi mkuu wa kampuni hiyo, Dennis Mullenburgh, amesema kuwa pesa hizo zitatolewa kwa kipindi cha miaka kadhaa ijayo ingawa hakutoa utaratibu utakaofuatwa.
Boeing inaendelea kuchunguzwa na taasisi mbalimbali na inakabiliwa na takribani kesi 100 zilizowasilishwa na familia za waathiriwa wa ajali hizo mbili, ambapo jumla ya watu 346 walipoteza maisha yao kwenye ajali hizo mbili.