Kaimu Waziri wa Afya nchini Ukraine, Ulana Suprun ametoa mtazamo wake kuhusu mapendekezo ya kutungwa kwa sheria inayokataza matusi na lugha chafu kwenye vyombo vya habari na mikutano ya hadhara akisema haina umuhimu.
Suprun amesema anaamini kuwa matusi huleta afya na kwamba katika kesi kadhaa ambazo watu hutukanana inaonekana kuwa wana mawasiliano mazuri ya kihisia kati yao.
Kwa mujibu wa BBC, Sheria hiyo imewalenga hasa wanasiasa na viongozi wa Serikali na inapendekeza faini ya hadi $49 kwa watakaokiuka.
Hata hivyo, kwenye mitandao ya kijamii watu wengi wameanza kuonesha mzaha na utani wakidai kuwa kama sheria hiyo itatungwa rasmi kuna kila dalili kuwa watatenga baadhi ya maeneo ambayo matusi yatakuwa yanaruhusiwa.
“Mimi nadhani watajenga jumba moja kubwa ambalo litakuwa maalum kwa ajili ya watu kutoleana matusi au kutukana ili kuondoa hasira zao bila kupigwa faini,” aliandika mtumiaji mmoja wa mitandao ya kijamii.
Sheria hiyo iko kwenye mchakato wa Bunge na inapitiwa na Kamati Maalum ya Bunge la nchi hiyo.