Kijana mmoja aliyefahamika kwa jina la Allan Kiluvya ambaye anatajwa kuwa ni msaidizi wa Waziri mstaafu wa Mambo ya Nje wa Serikali ya awamu nne, anatajwa kupotea baada ya kuchukuliwa na watu wasiojulikana usiku.
Tukio hilo limetokea usiku wa jana alipokuwa na baadhi ya marafiki zake katika eneo la Mbezi jijini Dar es salaam.
Kwa mujibu wa mtu wake wa karibu ambaye amefahamika kwa jina moja tu la Magreth, amesema kuwa mara ya mwisho yeye na Allan walikuwa pamoja wakitokea eneo la starehe, kabla ya kutokea kwa watu hao 7, wakiwa kwenye gari aina ya Land Cruiser ambayo ndiyo ilimchukua na kuondoka naye.
Aidha Magreth amesema kuwa tayari wameshatoa taarifa za awali kwa Jeshi la Polisi kwa ajili kuanza kwa uchunguzi wa kupatikana kwa Allan Kiluvya.
Kwa upande wake Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kipolisi wa Kinondoni, Mussa Taibu amesema kuwa tayari wameshapata taarifa za tukio hilo kutoka kwa ndugu zake Allan na wao wanaendelea kulifuatilia.,
“Tumepata taarifa za tukio hilo kutoka kwa ndugu zake Allan, na sisi tunaendelea kulifuatilia kujua ni kwa namna gani alichukuliwa lakini siwezi kusema ametekwa kwa sababu bado hatujathibitisha,”amesema Kamanda Taibu.