Waziri wa Maji, Prof. Makame Mbarawa amefanya ziara ya kikazi wilayani Missenyi Mkoani Kagera kukagua miradi ya maji pamoja na kukagua ujenzi mpya wa mradi mkubwa wa maji katika mji mdogo wa Kyaka kufuatia agizo lililotolewa na Rais Magufuli.
Akiwa njiani akitokea wilayani Karagwe alipokuwa mapumzikoni Rais Magufuli alisimama katika mji mdogo wa Kyaka kwaajili ya kusalimiana na wananchi waliojitokeza kumsalimia ndipo walipomwambia kuna kero ya maji ambayo imekuwepo hapo kwa miaka mingi hali iliyomfanya, Rais Magufuli kumpigia simu Waziri Mbarawa na kumtaka kufika katika mji huo kutatua kero hiyo.
Waziri Mbarawa akiwa wilayani Missenyi ameambatana na wataalamu kutoka Mamlaka ya Maji na Usafi wa Mazingira Mwanza na kukagua chanzo ambacho kitakuwa kinazalisha maji ambayo yatasambazwa katika maeneo ya Kyaka, Bunazi, Mutukula kwa kuanzia na baadaye yatapelekwa katika vijiji vya kata za Kakunyu na Bubale.
Akizungumza na wananchi waliojitokeza katika mji wa Kyaka, waziri Mbarawa amewahakikishia wananchi hao kuwa ndani ya miezi mitano kama Rais alivyoagiza maji yatakuwa yanatoka ili kuondoa kabisa kero hiyo.
“Nimekuja hapa na timu ya wataalamu kutoka BUWASA NA MUWASA kuanza kutekeleza agizo la Rais alilolitoa hapa, niwahakikishie wananchi maji yatapatikana na tutatumia chanzo hiki cha mto Kagera, ninachowaomba tuwe wavumilivu na tutoe ushirikiano wakati wa utekelezaji wa mradi huu, na nimeagiza vibarua wote watokee hapa Kyaka,”amesema Prof. Mbarawa
Kwa upande wake mkuu wa wilaya Missenyi, Canal Denis Mwila amemweleza waziri Mbarawa kuwa katika wilaya hiyo yapo maeneo ambayo tayari kwa jitihada zake yameshaanza kutoa maji ingawa changamoto ya maji katika wilaya hiyo ni kubwa kulingana na mahitaji yaliyopo.
Hata hivyo, waziri Mbarawa akiwa wilayani humo amekutana na halmashauri kuu ya CCM ya wilaya hiyo na kuwahakikishia wanaccm kutembea kifua mbele kwakuwa serikali yao inaendelea kutekeleza Ilani ya uchaguzi na kuwataka kuwafikishia ujumbe wananchi wa kazi zinazofanywa na serikali yao.