Naibu Waziri wa Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Mwita Waitara amewaonya wanachama wa chama cha Mapinduzi (CCM) wanaoendelea kukihujumu chama hicho waache mara moja.
Ameyasema hayo mkoani Njombe ambapo amesema kuwa amesikitishwa sana na kitendo cha baadhi ya wanachama wa aina hiyo kwa kuwa wamekuwa wakijaribu kurudisha nyuma jitihada za kuyafikia maendeleo ya chama hicho.
“Hauwezi kuwa mbunge wa chama cha mapinduzi, unaingia kwenye vikao vya CCM halafu unaipinga serikali huko nje, hauwezi kuwa salama, wenzetu Ulaya huwa wanaua nenda China kafanye mambo hayo, utaona kitakachokupata,”amesema Waitara
Waitara amesema kuwa huwezi kuwa mbunge wa chama cha mapinduzi, unahudhuria kwenye vikao vya chama, watu wanapanga mikakati halafu ukiwa mtaani unatoa siri zote, unakihujumu chama kwa kutoboa siri hivyo unatakiwa kuwajibishwa mapema.
Akizungumzia upande wa watumishi wa umma Waitara ametoa wito wa kumuunga mkono Rais Magufuli kutokana na juhudi kubwa anazozifanya kwa Watanzania.
“Kwa mtu mstaarabu anayejua uongozi maana yake nini, siwezi kukubali uteuzi nikaenda nikala kiapo, nikapewa majukumu, nikapewa na gari nikapewa na posho nikapewa na mshahara halafu nikakaa kwenye vijiwe nikamtukana rais, hivi unakuwa unaakili kweli,”amehoji Waitara