Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Nchini (TPA), Mhandisi Deusdedit Kakoko amezitaka Nchi za Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) kuunganisha nguvu ya pamoja katika kuimarisha miundombinu ya Reli, Barabara, Bandari pamoja na Mawasiliano ili kukuza sekta ya viwanda katika Mataifa hayo.
Ameyasema hayo jijini Dar es salaam wakati wa mjadala wa wataalamu uliojadili umuhimu wa sekta ya miundombinu katika ujenzi wa uchumi wa Viwanda katika Nchi Wananchama wa SADC, katika Maonesho ya Nne ya Wiki ya Viwanda kwa Nchi za SADC yanayoendelea Jijini Dar es Salaam.
Amesema kuwa kwasasa Tanzania imekuwa nchi ya mfano katika nchi za Ukanda huo, kwa kuwa imekuwa kitovu cha usafirishaji wa bidhaa na malighafi mbalimbali katika nchi za SADC, hatua iliyotokana na mikakati mbalimbali iliyowekwa na Serikali ya Awamu ya Tano katika kuimarisha Bandari, Reli na mtandao wa barabara.
“Zipo Nchi chache ndani ya SADC ikiwemo Afrika Kusini ambazo tayari zimepata mafanikio makubwa katika miundombinu yake ikiwemo Bandari ya Durban, hivyo mkutano huu unakuwa chachu kwa Mataifa yote kuweza kubaini changamoto zilizopo ili kuhakikisha tunakuwa na mkakati wa pamoja wa kutuvusha hapa tulipo,”amesema Kakoko.
Aidha, ameongeza kuwa ili kufikia mafanikio hayo Serikali za SADC hazina budi kuweka msisitizo katika kuziwezesha sekta binafsi ikiwemo mashirika ya maendeleo ya kimataifa kuwekeza katika miradi mbalimbali ya miundiombinu pasipo na kuweka masharti magumu kwa serikali, kwani kwa kufanya hivyo kutasaidia kuleta manufaa kwa wananchi walio wengi.
Kwa mujibu wa Kakoko amesema kuwa Serikali kupitia TPA imeanza kuchukua hatua mbalimbali katika kuimarisha kiwango cha ushindani na Bandari nyingine kubwa Barani Afrika na hivyo kuweza kukuza uchumi wa Nchi pamoja na kuwa kichocheo muhimu katika maisha ya wananchi.
Hata hivyo, Kakoko ameongeza kuwa miundombinu ya nchi za SADC kwasasa si mizuri kwa kuwa zimekuwa zikitumia gharama kubwa za fedha kwa ajili ya kugharamia miundombinu, hivyo ni wajibu wa Mashirika na Taasisi za umma na binafsi kujitokeza ili kusaidia uboreshaji na ujenzi wa miundombinu hiyo na hivyo kurahisisha uzalishaji wa bidhaa mbalimbali.