Mbio za mwenge wa uhuru kitaifa mwaka 2019 zimeshindwa kuweka jiwe la msingi katika ujenzi wa mradi wa maji kijiji cha Kidegembye jimbo la Lupembe wilayani Njombe mkoani Njombe.
Akizungumza na wananchi mara baada ya kukagua na kupitia nyaraka za ujenzi wa mradi huo amesema mwenge wa uhuru umeshindwa kuweka jiwe la msingi katika mradi huo kutokana na kubaini ukiukwaji wa utaratibu wa ujenzi.
“Baada ya kufanya uchunguzi wa kina, tumeona ‘chest’ ya nondo milimita nane haijapimwa lakini pia zege ya katikati haijapimwa, sambamba na hilo kwenye ‘pampu house’ zege imetumika na haijapimwa kwa hiyo maana yake hapa utaratibu wa kiujenzi umekiukwa,hivyo basi mbio za mwenge wa uhuru kitaifa hazitoweza kuweka jiwe la msingi katika mradi huu”alisema Mzee Mkongea
Aidha amesema licha ya kuwa Mwenge wa uhuru umeshindwa kuweka jiwe la msingi katika mradi huo, bado maji katika mradi yapo safi na salama na kuomba wananchi kuyatumia.
“Lakini maji yapo safi na salama ndugu wananchi muweze kuyatumia hayana shida yoyote,ambayo yamejitokeza hapa ni kwa wataalamu kuto kuweza kusimamia vizuri kwasababu hizi ni fedha za wananchi lazima zisimamiwe kipengele hadi kipengele”aliongezakiongozi wa mbio za mwenge
Katika hatua nyingine kiongozi huyo wa mbio za mwenge amemuagiza mkuu wa wilaya ya Njombe, Ruth msafiri, kumkabidhi taarifa ya mradi huo afisa Takukuru na kuichunguza kwa umakini na kuipeleka nakala hiyo baada ya wiki mbili makao makuu ya Takukuru.
Awali akisoma taarifa ya mradi huo Injinia wa maji halmashauri ya wilaya ya Njombe, Rajabu Yahaya kwa niaba ya mkurugenzi, amesema hali halisi ya utekelezaji wa mradi huo umefikia asilimia 90% ya kukamilika ambapo mpaka sasa wananchi wanapata huduma ya maji huku mradi huo ukiwa umeanza kutekelezwa machi 7,2018 na mkandarasi MSSTC construction limited kwa gharama ya shilingi bilioni moja.
Takribani miradi sita imekaguliwa na kufunguliwa na mbio za mwenge wa uhuru kitaifa wilayani Njombe mkoani Njombe huku kiongozi wa mbio za mwenge akitoa pongezi kwa halmashauri hiyo katika utekelezaji wa miradi.