Oktoba 9, 2019 Takukuru imeieleza mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jinsi ilivyomkamata mhadhiri msaidizi wa Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT), Samson Mahimbo mwenye umri wa miaka 68 akiwa mtupu akimtaka kingono mwanafunzi wake Victoria Faustine kwenye nyumba ya kulala wageni.
Hayo yameelezwa na wakili wa taasisi hiyo ya kuzuia na kupambana na Rushwa nchini Tanzania, Faraja Salamba wakati akimsomea maelezo ya awali mshtakiwa huyo mbele ya Hakimu mkazi mkuu, Huruma Shahidi.
Amedai kuwa Januari 5 na 11, 2017 mshtakiwa alitumia madaraka yake vibaya kuomba rushwa ya ngono baada ya kumpigia simu mwanafunzi wake Victoria Faustine na kumsisitiza wakutane katika baa ya Shani.
Ambapo Victoria aliitikia wito kukutana na mhadhiri Samson ambaye alikuja na mtihani wa marudio wa somo alilokuwa akifundisha na majibu alimpa, alipomaliza akasahihisha na kumpa alama ya 67.
Inadaiwa kuwa mara baada ya Victoria kumaliza kufanya mtihani huo na kusahihishiwa walihamia baa nyingine ya Camp David na kunywa pombe na mshtakiwa kuchukua chumba.
Mahakama hiyo imeelezwa kuwa walipoingia chumbani mshtakiwa alivua suruali na kubaki na nguo ya ndani na kumkumbatia mwanafunzi huyo.
Salamba amesema wakati mhadhiri huyo akimvua nguo mwanafunzi huyo, mlango uligongwa na Victoria alikwenda kufungua na waliingia maofisa wa Takukuru.
Aidha moja ya Profesa amewahi kuhojiwa jina lake limehifadhiwa amesema kuwa moja ya sababu kubwa ni pale ambapo mhadhiri anapotamani kutumia nafasi yake vibaya kujinufaisha na ngono huku mwanafunzi nae akitamani kupata alama za bure mara nyingi imekuwa ikiwaponza.