Wakulima wa kanda ya kati inayohusisha Mikoa ya Dodoma, Singida na maeneo jirani wameshauriwa kuutumia vyema msimu wa mvua za masika zinazotarajiwa kuanza wiki ya kwanza hadi ya pili ya mwezi Novemba 2019.
Ushauri huo umetolewa na Meneja wa Mamlaka ya hali ya hewa (TMA) kanda ya kati Izidor Kirenga jana, wakati akizungumzia juu ya ujio wa mvua hizo na kudai kuwa zitaendelea hadi wiki ya kwanza na ya pili ya mwezi Aprili 2020.
Amesema tayari taarifa juu ya ujio wa mvua hizo imeshasambazwa kwa maafisa ugani wa maeneo mbalimbali ambao watakuwa na jukumu la kuwashauri wakulima kujiandaa na upandaji wa mazao mbalimbali ambayo yanastahimili hali ya hewa ya ukanda wa kati.
“Mvua hizi za masika kwa ukanda wa kati yaani mikoa ya Singida na Dodoma zinatarajia kuanza wiki ya kwanza au ya pili ya mwezi Novemba 2019 kuendelea hadi wiki ya kwanza au ya pili ya mwezi April, 2020 hivyo kwa wakulima wazitumie vyema kupanda mazao,” amefafanua Kirenga.
Amesema kwa kawaida maeneo ya kanda ya kati mvua hunyesha kati ya milimita 500 hadi milimita 600 huku akibainisha kuwa kiwango cha mvua inayonyesha si muhimu bali kinachotakiwa ni kujua mtawanyiko wake
unaanza wakati gani na kuishia kipindi kipi.
Hata hivyo mbali na uhimizaji wa shughuli za kilimo Kirenga pia mewataka wazazi kuchukua tahadhari kwa watoto wao ili kujikinga na majanga yanayoweza kuzuilika kwa kuchukua tahadhari mbalimbali za radi, madimbwi ya maji mitaro na mashimo marefu.
“Wakati wa mvua za masika huwa kuna mambo mengi ya kuzingatia ili kuokoa majanga yanayoweza kutokea wazazi wanatakiwa kuwa makini na watoto kwa kuwa karibu nao ili wasije pata matatizo kwa kuangalia maeneo wanayocheza isiwe kwenye mifereji au mashimo yaliyojaa maji,” amebainisha meneja huyo wa TMA.
Oktoba 10, 2019 Mkurugenzi mtendaji wa Mamlaka ya hali ya hewa nchini Dkt. Agnes Kijazi aliwasilisha taarifa ya mwenendo wa hali ya hewa kuanzia mwezi Novemba na kutoa tahadhari kwa wadau wa sekta ya kilimo, usafiri wa anga, nchi kavu, maliasili na utalii, maji na menejimenti ya maafa.