Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kimetangaza kuwa hakitashiriki katika uchaguzi wa Serikali za Mitaa utakaofanyika Novemba 24 mwaka huu.
Mwenyekiti wa chama hicho, Freeman Mbowe ametoa tamko hilo leo, Novemba 7, 2019 jijini Dodoma, baada ya Kamati Kuu ya chama hicho kufanya kikao cha dharura.
Mbowe amesema kuwa wamefikia uamuzi huo baada ya kutoridhishwa na utaratibu wa kuwaondoa wagombea wao katika maeneo mbalimbali nchini.
Alisema kuwa zaidi ya asilimia 80 ya wagombea wa chama hicho wameenguliwa kwa kile kilichoelezwa kuwa wamekosa sifa au fomu zao zimekosewa.
“Katika mzingira hayo viongozi wa chama kupitia Kamati Kuu wameona sio busara kubariki uchaguzi wa kihuni; na kuendelea kushiriki uchaguzi huu ni kubariki uhuni,” alisema Mbowe.
Mwenyekiti huyo wa Chadema amesema kuwa hata wale wagombea ambao walikuwa wamekata rufaa baada ya kutolewa kwa maelezo kuwa wamekosa vigezo wasiendelee na hatua hiyo.
Kufuatia uamuzi huo, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Suleiman Jafo amewatumia ujumbe Chadema akieleza kuwa uamuzi waliouchukua unawanyima haki wagombea wao ambao baadhi [walioenguliwa] rufaa zao zitaamlia hivi karibuni.
“Ingawa hii ni haki, lakini nimeshangazwa na kujitoa kwao kwa sababu kila kitu kiko wazi. Kanuni haijamfunga mtu yeyote kudai haki ya kukata rufaa. Huenda leo uamuzi wa rufaa zilizokatwa na baadhi ya wagombea ukatolewa lakini nashangaa wao kujitoa,” alisema Waziri Jafo.
Uchaguzi wa Serikali za Mitaa umepangwa kufanyika Novemba 24, 2019 nchi nzima na unasimamiwa na TAMISEMI.