Mtoto wa miezi sita wilayani Hai mkoani Kilimanjaro, Junedi Mbaga amefariki muda mfupi baada ya kufanyiwa tohara kwenye zahanati binafsi katika mazingira yenye utata.
Umetokea mvutano juu ya kifo cha mtoto huyo kwani ndugu wa mtoto wanaamini kuwa kichanga chao kimefariki kutokana na tohara aliyofanyiwa, huku daktari aliyehusika akidai mtoto alibanwa na makohozi hivyo alikosa pumzi na kupoteza maisha.
Imeelezwa kuwa ndugu wa mtoto wanaomba waziri wa Afya, maendeleo ya jamii, jinsia, wazee na watoto, Ummy mwalimu na Jeshi la polisi kusaidia kuchunguza kifo hicho.
Bibi wa marehemu, Zuhura Msangi amesema kuwa mnamo oktoba 24 yeye na kijana wake, Murtaza Mbaga pamoja na mkewe walimpeleka mtoto huyo zahanati na walitoa Tsh. 20,000 ili kupata huduma hiyo.
Ameeleza kuwa, alipoingizwa chumba cha upasuaji mtoto alichomwa sindano na akalia sana halafu akalala.” Dokta aliendelea na kazi yake na alipomaliza alimshona”
Ameendelea kueleza kuwa baada ya kumaliza upasuaji “Alimpiga piga chini ya tumbo na kusema tumbebe na tukae pembeni ili ahudumie wagonjwa wengine tulifanya hivyo”
Lakini baada ya nusu saa amesema mtoto alifumbua macho lakini alikuwa akihema kwa shida hivyo wakamuagiza kwa daktari ambaye alijaribu kumvuta makohozi lakini alishindwa kwani hakuwa na vifaa.
Walipokuwa njiani mtoto alifumbua macho na kuhema kwa nguvu na kufumba tena macho na hakuhema tena hadi walipofika hospitalini na kuambiwa mtoto tayari amefariki.
Mmiliki wa zahanati hiyo ya Boma Health care, Dkt. Chrispin Mushi, ameliambia gazeti la mwananchi kuwa mtoto huyo hajafariki kwasababu ya tohara waliyomfanyia.
“Ni kweli alifanyiwa tohara katika zahanati yetu na alizinduka na kuanza kucheza vizuri” amesema Dkt. Mushi.
Na kubainisha kuwa mtoto huyo alifariki kwa kukosa hewa baada ya kupaliwa na makohozi wakati akilia.