Watu milioni tano hasa jamii ya waishio vijijini  wamepatiwa elimu ya msaada wa kisheria hadi kifikia mwishoni mwa mwaka 2019 hali iliyopelekea kupungua kwa migogoro mbalimbali na  msongamano wa kesi mahakamani nchini.

Hayo yamebainishwa na Afisa mradi mwandamizi wa Legal Services Facility (LSF), Fortunata Kitokesia mkoani Dodoma katika kongamano la kitaifa lililowakutanisha wasaidizi wa wakisheria 400 wa Tanzania bara na Visiwani.

Amesema wanasheria wengi nchini wamekuwa wakiishi mjini kitu ambacho kimewafanya kusahau kuwa kundi kubwa la jamii lililopo pembezoni ndilo lenye uathirika wa migogoro mbalimbali na dhuluma dhidi ya haki zao.

“Wasaidizi wa kisheria  wamekuwa ni watu wakuleta utulivu na amani nchini na hasa kusaidia katika suala zima la kukuza na kuimalisha maendeleo ya taifa hivyo wasiishie mijini pekee bali watambue kuna watu kule vijijini wana uhitaji wa huduma za kisheria,” amsema Fortunata .

Aidha ameongeza kuwa wananchi ambao wamepatiwa elimu ya msaada wa kisheria tayari wamekuwa wadau wazuri kutokana na uwajibikaji wao kwa wengine sambamba na kujua haki zao binafsi zinazowasaidia kukabiliana na vitendo vya dhuluma.

Kwa upande wake mwakilishi wa mashirika yasio ya kiserikali kutoka ofisi ya Rais tawala za mikoa na serikali za mitaa (TAMISEMI), Dennis Londo amesema wasaidizi wa kisheria ndio wadau wakubwa wa haki na wamekuwa wakijitahidi kuhakikisha haki inapatikana katika jamii.

Hata hivyo amefafanua kuwa haki ndio msingi wa maendeleo na kwamba wasaidizi wa kisheria waamekuwa wakipambana usiku na mchana kuhakikisha mwenye haki anapata stahiki yake kulingana na utaratibu wa kisheria unavyoongoza.

“Naomba nitoe rai kwa wasaidizi wa kisheria kuhakikisha wanashirikiana na viongozi wa chini wa serikali za mitaa ili kila mwenye haki apate haki yake maana kwa kufanya hivyo ni wazi kuwa utaratibu wa ushirikishwaji kisheria utakua umefuata misingi husika,” amebainisha Londo.

Naye msaidizi wa sheria kutoka mkoa wa Kilimanjaro Getrude Tery amesema wamejikita katika makundi ya kinamama wajane ambao wameonekana kuwa na changamoto ya umiliki mali hasa pale wanapofiwa na wenza wao.

Kikongwe adai kuporwa ardhi yenye kaburi, vitindi vya ulanzi, aiangukia Serikali
Ushirikina Tabora: Polisi yataka ushirikiano, mwisho wa mwaka