Kamishna wa maadili, Jaji msaafu Harold Nsekela amesema kuanzia mwaka ujao, ujazaji na urejeshaji wa tamko la rasilimali na madeni kwa viongozi wa umma utafanyika kwa njia ya mtandao.
Akizungumza Jijini Dodoma, Jaji Nsekela amesema hatua hiyo imetokana na maombi ya viongozi wengi wakiwamo mabalozi, ambao kwao wanaona ni rahisi kujaza na kurejesha kwa njia ya mtandao.
“Kutokana na mabadiliko ya teknolojia, kuanzia Januari mwakani, tutaanza kutumia mtandao katika kujaza na kurejesha tamko la rasilimali na madeni kwa viongozi wa umma, tulikuwa tufanye majaribio ya mfumo Desemba hii ili kuangalia ufanisi wake lakini kuna masuala kadhaa ya kiufundi yaliyokwamisha” amesema Jaji Nsekela.
ameeleza kuwa kutokana na hilo waliamua kujaribu ufanisi wa mfumo huo kwa kuwatumia wafanyakazi wa ndani ya Sekretarieti ya maadili na ulifanya kazi vizuri hivyo watatangaza rasmi kuanza kutumia mfumo huo baada ya kukamilisha masuala ya leseni.
Alipozungumzia juu ya tathimini ya hali ya urejeshaji wa tamko la rasilimali na madeni kwa viongozi wa umma amesema imebaki wiki moja lakini ni asilimia 17 wamekamilisha.
Hivyo ameagiza asilimia 83 ya viongozi wa umma ambao hawajatekeleza takwa hilo la kisheria kufanya hivyo kabla muda wa mwisho haujafika.