Jeshi la Polisi mjini Garissa limeanzisha juhudi za kuwaokoa wafanyabiashara, Abdulahi Isaack Harun na Abdi Hassan wanaoaminika kutekwa nyara jana asubuhi na wanachama wa kundi la Al-shabaab.
Imeelezwa kuwa watu hao walikuwa wanasafirisha ‘miraa’ kutoka Garissa kwenda Liboi, lakini walipofika Wardeglo Dam, walitekwa nyara na inashukiwa wamepelekwa Somalia.
Magari waliyokuwa nayo wafanyabiashara hao yalionekana mara ya mwisho eneo la Osman Baret kwenye mpaka wa Abdisugow na Gubahadhe mpakani mwa Somalia.
Hayo yanajiri wiki mbili tu baada ya Al-shabaab kuteka nyara basi moja kutoka Garissa na kuwaua watu 10 wakiwemo maafisa wa polisi 6.