1. Kushiriki kwa Taifa Stars AFCON baada ya miaka 40.

Image result for taifa stars yapoteza dhidi ya kenya afcon 2019

Baada ya mashabiki watanzania kusubiri kwa muda mrefu timu yao kutinga kwenye fainali za mataifa ya Afrika, mwaka 2019 Taifa Stars ilibahatika kuwa miongoni mwa mataifa 24 yaliyoshiriki fainali hizo ziliozounguruma nchini Misri.

Stars ilipangwa kundi C lililokuwa na timu za Senegal, Kenya na mabingwa Algeria. Lakini kwa bahati mbaya Stars haikufanikiwa kushinda mchezo hata mmoja na kujikuta wakimaliza mkiani mwa kundi hilo na kuondolewa kwenye hatua ya makundi.

Kwa watanzani ilikua ni faraja kubwa sana kwao kwa timu yao kushiriki fainali za AFCON baada ya miaka 40 kupita, tunaamini morari na somo timu yetu iliyopata kwenye fainali za mwaka huu, itakuwa ni hamasa kwa kuhakikisha inapambana ili ifuzu tena kwenye fainali za 2021.

  1. Messi kutwaa Ballon d’or

Image result for lionel messi ballon d'or 2019

Mshambuliaji mchachari wa FC Barcelona na timu ya taifa ya Argentina, aliandika historia ya kuwa mchezaji wa kwanza duniani kutwaa tuzo ya Ballon d’or kwa mara ya sita.

Hatua ya mshambuliaji huyo ya kutwaa mara sita tuzo ya Ballon d’or, ilidhihirisha kuwa mbele ya mpinzani wake Cristiano Ronaldo, ambaye amesaliwa na tuzo tano za Ballon D’or.

Kwa mwaka huu 2019, Messi alipambanishwa na Cristiano Ronaldo na beki wa Liverpool Van Djik.

Sherehe za kutangazwa kwa mshindi wa tuzo hii kwa mwaka 2019 zilifanyika Théâtre du Châtelet, Paris, Ufaransa.

  1. Liverpool kutwaa mataji matatu mkubwa (Ligi ya mabingwa Ulaya, UEFA Super Cup Na Klabu bingwa duniani).

Image result for champions league, super cup and FIFA club champions for liverpool

Haijawahi kutokea kwa klabu ya England(Uingereza) kufikia mafanikio makubwa kama iliyoyapata klabu ya Liverpool kwa mwaka huu 2019.

Ilionyesha ukomavu kwenye michuano ya ligi ya mabingwa barani Ulaya kwa kutwaa ubingwa wa michuano hiyo, kufuatia ushindi waliouvuna kutoka kwa Tottenham Hotspurs, kwenye fainali iliyochezwa Juni Mosi 2019, Mjini Madrid-Hispania katika uwanja wa Wanda Metropolitano unaomilikiwa na klabu ya Atletico Madrid.

Mabao mawili yaliyofungwa na Mohamed Salah na Divock Okoth Origi, ndio yalikua sehemu ya mafanikio ya klabu hii ya mjini Liverpool pale nchini England.

Kama hiyo haitoshi, mnamo 14 Agosti 2019, Klabu ya Liverpool waliuendeleza moto wao wa ushindi katika mchezo wa UEFA Super Cup dhidi ya ndugu zao kutoka England, Chelsea, ambao uliashiria kufunguliwa rasmi kwa msimu wa 2019/20 kwa michuano ya barani Ulaya.

Liverpool FC hawakupata ushindi kirahisi katika mpambano huu uliofanyika kwenye dimba la Vodafone Park, mjini Istanbul-Uturuki, baada ya kwenda sare ya mabao mawili kwa mawili, na kuamuriwa mikwaju ya penati ipigwe.

Katika hatua hiyo majogoo wa jiji waliibuka kidedea kwa penati tano kwa nne.

Desemba 21, 2019 wababe hawa wa ligi ya England kwa mwaka huu, walifanikiwa kutwaa taji la tatu lenye umaarufu mkubwa dunia la klabu bingwa duniani (FIFA Club World Cup) kwa kuwafunga mabingwa wa ukanda wa kusini mwa Amerika Flamingo.

Liverpool FC walipata ushindi katika mpambano huo uliounguruma kwenye uwanja wa Khalifa International uliopo mjini Doha-QATAR, huku bao la ushindi likifungwa na kiungo mshambuliaji kutoka Brazil, Roberto Firmino Barbosa de Oliveira, dakika ya 99.

  1. Simba SC kutinga robo fainali ya ligi ya mabingwa Afrika.

Image result for simba yatinga robo fainali ligi ya mabingwa afrika

Mwaka 2019 ulikua mwaka muhimu na utaendelea kukumbukwa na mashabiki wengi wa soka la Tanzania hususan wale wa klabu ya Simba SC, kufuatia timu yao kutinga hatua ya robo fainali ya michuano ya ligi ya mabingwa barani Afrika kwa kuifunga Nkana FC ya Zambia jumla ya manne kwa matatu.

Mchezo wa kwanza wa hatua ya mtoano wa michuano ya ligi ya mabingwa barani Afrika kati ya wawili hao ulipigwa mjini Kitwe-Zambia katika uwanja wa Nkana mnamo Desemba 16 – 2018 na wenyeji walichomoza na ushindi wa mabao mawili kwa moja.

Siku saba baadaye yaani Desemba 23 – 2018, miamba hiyo ikacheza mchezo wa mkondo wa pili kwenye dimba la Taifa Dar es Salaam, na hapo ndipo wana Msimbazi walipowafurahisha mashabiki wao kwa kulipa kisasi na kuiondosha Nkana FC kwa kuibanjua mabao matatu kwa moja.

Baada ya hapo Simba ilijikatia tiketi ya kwenda moja kwa moja katika hatua ya makundi ambapo ndio lilikua kusudio lao, na walipangwa kundi D lililokua na timu za Al Ahly ya Misri, AS Vita ya DR Congo na JS Saoura ya Algeria.

Kwa mipango na mikakati Simba walifanikiwa kushinda michezo yao yote ya nyumbani na kupoteza michezo ya ugenini, na mwishowe waliambulia alama 9, zilizowavusha na kutinga hatua ya robo fainali.

Bao lililowavusha Simba kutinga hatua hiyo kwa mwaka 2019 lilifungwa na kiungo kutoka Zambia Cletus Chota Chama dhidi ya AS Vita kwenye mchezo uliopigwa mjini Dar es Salaam, Machi 16.

Katika mchezo huo Simba walichomoza na ushindi wa mabao mawili kwa moja na bao la kwanza lilifungwa na Mohamed Hussein Tshabalala.

Katika hatua ya robo fainali Simba SC walipangwa kukutana na TP Mazembe ya DR Congo, katika mchezo wa mkondo wa kwanza uliochezwa Dar es salaam Aprili 6, Simba walishindwa kuunguruma nyumbani kwa kuambulia matokeo ya sare ya bila kufungana na walipokwenda mjini Lubumbashi Aprili 13, walichezea bakora nne kwa moja na kutupwa nje ya michuano hiyo ambayo ilimalizika kwa klabu ya Espérance de Tunis ya Tunisia kutwaa ubingwa.

  1. Beki wa Liverpool Virgil van Dijk kutwaa tuzo ya mchezaji bora Ulaya.

Image result for virgil van dijk wins uefa player of the year

Tangu aliposajiliwa na klabu ya Liverpool mwaka 2018 akitokea Southampton FC kwa dau la Pauni milioni 75, alionyesha utofauti mkubwa katika utetezi wa safu ya ulinzi ya majogoo hao wa jiji la Liverpool.

Muda wa Msimu wa 2018/19 ulivyokua unasogea kila shabiki duniani alimzungumza kwa mazuri, huenda ilikua ishara nzuri ya kufikia mafanikio aliyoyapata kwa mwaka huu tunaoumaliza kwa kutangazwa kuwa mshindi wa tuzo ya mchezaji bora wa bara la Ulaya.

Aliingizwa kwenye kinyang’anyiro cha kuwani tuzo hiyo ambacho kilele chake kilikua Agosti 29, baada ya kuonyesha umaridadi mkubwa katika michuano ya ligi ya mabingwa barani Ulaya huku akiwa sehemu ya kikosi cha Liverpool kilichotwaa ubingwa wa bara hilo kwa kuwafunga ndugu zao kutoka England (Tottenham Hotspurs).

Katika orodha ya mwisho iliyotolewa na UEFA ilionyesha Virgil van Dijk alikua akishindanishwa dhidi ya mshambuliaji wa FC Barcelona (Lionel Messi) na mshambuliaji wa Juventus (Cristiano Ronaldo).

Mlolongo wa upigaji wa kura na matokeo yaliyotangazwa ilionekana dhahir Virgil van Dijk ndio mshindi wa tuzo hiyo kwa kupata kura 305, akifuatiwa na Lionel Messi aliepata kura 207 na Ronaldo aliambulia kura 74.

  1. Kuibuka kwa shabiki wa Taifa Stars kutoka England (Bongo Zozo).

Image result for bongo zozo

Ilistaajabisha sana kwa soka la Tanzania kupata shabiki mwenye asili ya barani Ulaya (MZUNGU), Shabiki huyo alijizolea umaarufu wakati timu ya taifa ya Tanzania (taifa Stars) ilipokua ikishiriki fainali za mataifa ya Afrika (AFCON 2019) kule nchini Misri.

Licha ya Taifa Stars kushindwa kufurukuta kwenye fainali hizo kwa kufungwa michezo yote ya hatua ya makundi na kutupwa nje mapema, bado shabiki huyu anaeongea vyema lugha ya Kiswahili alionekana kuipenda timu hiyo, na ndipo vyombo vya habari vya hapa nyumbani vilipoanza kumfuatilia na baadae shirika kubwa la utangazaji duniani BBC likamsaka na kufanya naye mahojiano na kumuuliza kulikoni yeye ni raia wa England, lakini ameangukia kimapenzi kwa taifa ya Tanzania (Taifa Stars)?

Bongo Zozo ndio jina lake, na tangu kipindi hicho mpaka hii leo shabiki huyu aliejinasibu kuifahamu vyema Tanzania hasa mikoa ya Iringa na Kilimanjaro amejipatia umaarufu mkubwa hapa nchini, na ameahidi kuhudhuria kila mchezo wa Taifa Stars ima uwe wa nyumbani ama ugenini.

NI FAHARI KWA TANZANIA KUWA NA MTU HUYU NA IKIWEZEKANA TUMTHAMINI SANA.

  1. Taifa Stars kufuzu michuano ya CHAN baada ya miaka 10.

Image result for taifa stars yafuzu chan

Ilikua kama gundu kwa Taifa Stars kushiriki fainali za mataifa bingwa barani Afrika (CHAN) baada ya kufanya hivyo mara ya mwisho mwaka 2009 ilipokua ikinolewa na kocha kutoka Brazil (Marcio Baselio Maximo).

Miaka nenda rudi timu yetu ilijaribu kusaka nafasi ya kushiriki kwa mara ya pili fainali hizi zinazoshirikisha wachezaji wanaocheza ligi za ndani, lakini ilishindikana.

Ngoja ngoja ya machungu kwa mashabiki wa Tanzania ilimalizika mwaka huu 2019 kwa kuzifunga timu za Kenya na Sudan na kufanikiwa kutinga kwa mara ya pili fainali za CHAN.

Safari ya kufuzu ilitaka kufanana kama ilivyokua mwaka 2009, lakini kwa mwaka huo Tanzania iliziondoa Uganda, Kenya na Sudan.

Kikubwa tumshukuru Mungu tumefanikiwa kufuzu, na tukio hili linaingia katika matukio 10 bora ya michezo ya Dar24.

  1. Algeria kutwaa ubingwa wa Afrika.

Image result for algeria win afcon 2019

Timu ya taifa ya Algeria (Mbweha wa Jangwani) haikufikiriwa kama itaweza kutwaa ubingwa wa bara la Afrika katika fainali za AFCON zilizofanyika mwaka huu nchini Misri.

Zilitajwa timu tofauti kama mabingwa watarajiwa, lakini taifa hili la Afrika kaskazini halikutajwa kabisa na vyombo vya habari vya dunia.

Algeria waliokua wamepangwa kundi moja na Tanzania, walipambana vyema tangu mwanzo wa fainali hizo hadi mwisho, na hawakupoteza hadi walipoichabanga Senegal bao moja kwa sifuri katika mchezo wa mwisho.

Hatua ya kutwaa ubingwa wa Afrika, iliifanya nchi hiyo kufikisha mataji mawili ya bara hilo, kwa mara ya kwanza walifanya hivyo mwaka 1990.

  1. Kufariki kwa mwanachama mfurukutwa na mkereketwa wa klabu ya Young Africans Ibrahim Omar Akilimali.

Image may contain: 1 person, text

Unapozungumzia soka la Tanzania husana katika miaka ya hivi karibuni huwezi kuacha kumtaja Mzee Ibrahim Oma Akilimali.

Mzee huyu alisifika na kuzunguzwa kila kona ya soka la bongo kutokana na misimamo na busara zake pale lilipojitokeza suala la kuiyumbisha klabu ya Young Africans, ambayo alidai kuipenda katika maisha ya uhai wake hapa duniani.

Mzee Akilimali anakumbukwa kwa kauli yake ambayo ilisababisha kuzuia harakati za aliyekua mwenyekiti wa klabu ya Young Africans, Yusuph Mehboub Manji, za kutaka kukodishwa klabu hiyo kwa kipindi cha miaka kumi.

Alisema katika mkutano n a waandishi wa habari, “Klabu ya Young Africans Haikodishwi kama masufuria ya shughulini” na hapo ndipo alipoibua zogo kubwa dhidi ya wanachama waliokua wanamuunga mkono Manji, ambapo alionekana kama mpinga maendeleo ya klabu hiyo.

Sio tukio hilo tu ambalo Akilimali anakumbukwa katika utetezi wa klabu yake pendwa, bali alishiriki kumng’oa madarakani aliyekua mwenyekiti wa Young Africans, Loyd Nchunga akishirikiana na wazee wenzake wanaounda baraza la wazee wa Yanga.

Mzee huyualifariki dunia Disemba 14 – 2019 na kuzikwa kwenye makaburi ya Tandale kwa Mtogole na maelefu ya wadau wa soka jijini Dar es Salaam Desemba 15, 2019.

  1. Ushindi wa Bondia Hassan Mwakinyo dhidi ya Tinampay.

Image result for hassan mwakinyo dhidi ya tinampay

Mchezo wa masumbwi kwa Tanzania katika mwaka 2019, ulipanda na kama utakua na kipimo kizuri basi unaweza kuuweka katika nafasi ya pili kwa kupendwa na kufuatiliwa baada ya mchezo wa soka.

Kasi ya kupendwa na kufuatiliwa kwa ukaribu mchezo huu, ilichagizwa na hatua ya kufanya vyema kwa bondia kutoka jijini Tanga, Hassan Mwakinyo, ambaye alianza kutamba katika medani ya ndondi duniani pale umchapa bondia wa England Sam Eggington mwaka jana 2018.

Kwa mara ya kwanza mwaka 2019 Mwakinyo alipanda uingoni katika ardhi ya nyumbani kucheza pambano la kimataifa dhidi ya bondia kutoka nchini Ufilipino Arney Tinampey.

Wadau wa michezo nchini kote wakishirikiana na Serikali walikuwa na hamu ya kumuona Mwakinyo akipata ushindi katika pambano hilo, lililounguruma Uwanja wa Uhuru Novemba 29.

Mungu alijaalia Mwakinyo alimshinda mpinzani wake kwa point na kufanikisha lengo na madhumuni ya kuutangaza mchezo wa ndondi kwa wadau wa michezo wa ndani na nje ya nchi.

Daktari, muuguzi kizimbani kwa kutakatisha fedha na Utoaji mimba
Kenya: Wafanyabiashara wa miraa wahofiwa watekwa na Al- shabaab