Mkuu wa mkoa wa Mbeya, Albert Chalamila ametangaza kuifunga barabara inayounganisha mkoa wa Mbeya na Tabora kwa wiki mbili baada ya daraja la mto Lupa kuvunjika.
Akizungumza katika eneo hilo, Chalamila amewataka wananchi kutumia njia ya Makongorosi na MKwajuni kwenda Songwe na kutokea mjini Mbalizi mkoani Mbeya.
“Mimi kama mwenyekiti wa kamati ya ulinzi na usalama nichukue jukumu la kuifunga barabara hii kwanza kwa muda watu wanaokwenda Tabora au Mbeya mjini wazunguke Mkwajuni” amesema Chalamila.
Daraja la mto Lupa katika barabara kuu ya Mbeya – Tabora lilivunjika baada ya gari lenye uzito mkubwa kuliko uwezo wake kupita na kusabisha mawasiliano kati ya pande hizo mbili kukatika na kuleta maafa.
Hata hivyo uamuzi huo umetolewa huku tayari watu wawili ambao walikuwa kwenye basi walipojaribu kuvuka wa miguu kusombwa na maji.
Katika hatua nyingine RC Chalamila ameviagiza vyombo vya ulinzi na usalama kuweka ulinzi ili watu wasiruhusiwe kupita kwenye daraja hilo sambamaba na kuwaagiza wakala wa barabara nchini (TANROAD) kuweka uzio ili kuzuia watu wasivuke katika mtu huo.
“Kuna ongezeko la kilomita kama 50 hivyo kuanzia leo hakuna mtu kupita awe kwa miguu wala kwa gari hivyo niagize vyombo vya ulinzi kusimamia hili kuzuia watu wasipite hapa tena” amesisitiza Chalamila.
Aidha ameagiza kampuni inayomiliki gari lililokuwa limesababisha kuvunjika daraja kuangalia namna ya kujenga daraja hilo wakati ujenzi wa daraja kubwa ukiendelea.
Kwa upande wake Diwani wa kata ya Matundasi wilayani Chunya, Kimo Choga amesema kuvunjika kwa daraja hilo kumepelekea adha kubwa kwasababu shughuli za kijamii na kiuchumi zinazotegemea barabara hiyo zimesimama.