Baraza kuu la Umoja wa mataifa liliidhinisha bajeti yake ya dola bilioni 3.07 ambayo kwa mara ya kwanza inajumuisha fedha kwa ajili ya uchunguzi wa uhalifu wa kivita nchini Syria na Myanmar.
Bajeti hiyo ina ongezeko dogo kutoka ile ya mwaka 2019 ya dola bilioni 2.9. Ongezeko hilo ni kutokana na ujumbe wa ziada unaliowekwa katika sekretariati ya Umoja wa mataifa , hali ya maisha kupanda na marekebisho ya kiwango cha ubadilishaji fedha.
Kwa mara ya kwanza bajeti imetengwa kwa ajili ya uchunguzi nchini Syria na Myanmar, ambao hapo awali ulikuwa ukigharamiwa na michango ya hiari, lakini mwaka 2020 bajeti ya uchunguzi huo ipo katika bajeti ya sekretariati ya Umoja wa mataifa na itapatiwa michango ya lazima kutoka kwa matifa wanachama 193.
Hata hivyo bajeti ya matumizi ya Umoja wa mataifa ni tofauti kutoka bajeti ya mwaka kwa ajili ya operesheni za kulinda amani ya kiasi cha dola bilioni 6 ambazo ziliidhinishwa mwezi Juni 2019.