Jeshi la Polisi mkoa wa Tanga limewapa nusu saa pekee wakazi wa mitaa mbalimbali kusheherekea mkesha wa mwaka mpya na kutangaza atakaye kamatwa baada ya muda huo atajuta.
Kamanda wa Polisi mkoa wa Tanga, Edward Bukombe aliweka wazi msimamo huo wakati wa kikao chake na waandishi wa habari cha kuzungumzia na jeshi hilo lilivyojipanga kudhibiti vitendo vya uvunjifu wa amani wakati wa mkesha wa mwaka mpya.
“Tunawapa nusu saa pekee kwa maana ya kuanzia saa 6: 00 usiku hadi saa 6:30, wakazi wa mitaa mbalimbali kusherehekea bila kuchoma matairi, kurusha mawe, kulipua baruti na mafataki na baada ya hapo kila mmoja awe ameingia ndani kujipumzisha ili kupata nafasi ya kufanya ulinzi mitaani” amesema Bukombe.
Amesema mwaka huu ameamua kutangaza hali ya hatari mapema kwa sababu vijana wa mkoa wa Tanga hususani Jiji la Tanga wana kasumba ya kuadhimisha mwaka mpya kwa kuendesha vitendo vya kiahalifu na kuwahofisha wananchi walioko majumbani kwao.
Kamanda Bukombe amesema hadi kufika jana aliyekuwa ameomba na kupewa kibali cha kufyatua mafataki kwaajili ya kuadhimisha mkesha wa mwkaa mpya ni Hoteli ya Tanga Beach pekee na kwamba mwingine yeyote atakaye fanya hivyo atakamatwa.
Aidha amesema ameshakutana na wenyeviti wa Serikali za mitaa na kuwaeleza majukumu yao katika kulinda usalama wakati wa mkesha huo ili waweze kuwaelekeza wakazi wa maeneo yao.