Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) imetangaza kufanya uhakiki wa laini zote za simu zilizosajiliwa na kuwachukulia hatua za kisheria watu waliosajili laini kwa kutumia kitambulisho cha mtu mwingine.
Hatua hiyo imekuja siku chache baada ya baadhi ya watu kufungiwa huduma za simu kutokana na kutosajili laini zao za simu kwa alama za vidole kwa mujibu wa sheria.
Hata hivyo, uhakiki huo utawahusu wale waliosajili laini zao kwa kutumia kitambulisho tofauti ambapo wote watachukuliwa hatua za kisheria.
“Ikumbukwe kwamba kusajili laini ya simu kwa kutumia kitambulisho cha mtu mwingine ni kosa sanjari na kupewa laini iliyosajiliwa na mtu mwingine,” imeeleza taarifa ya Mamlaka hiyo.
Pamoja na mambo mengine, TCRA imesema waombaji wapya wa laini za simu wataendelea kusajiliwa muda wote kwa kutumia kitambulisho cha taifa na kuhakikiwa kwa alama za vidole ambapo huduma hiyo ni endelevu.
Imesema, kundi la kwanza waliozimiwa laini zao ni watu 656,091 ambao wana vitambulisho vya Taifa au Namba lakini hawajasajili laini zao.