Baadhi ya shule nchini Malawi zimefungwa na wanafunzi wamerejeshwa makwao siku chache kabla ya mahakama nchini humo kutoa uamuzi juu ya kesi ya uchaguzi.
Upinzani nchini humo ulifungua kesi mahakamani kupinga ushindi wa Rais Peter Mutharika ambaye amechaguliwa kuongoza nchi hiyo kwa muhula wa pili.
Mahakama nchini humo inatarajiwa kutoa uamuzi wa kesi hiyo Jumatatu, Februari 3 mwaka huu.
Mbali na shule hizo kufungwa kutokana na hofu ya kuwepo kwa vurugu katika siku hiyo, kampuni kubwa za mabasi ya abiria pia zimetangaza kuwa hazitotoa huduma ya usafiri.
Kumekuwapo na migogoro ya kisiasa, hofu na maandamano nchini Malawi tangu uchaguzi mkuu ulipofanyika Mei 2019.
Waziri wa habari wa nchi hiyo amewataka watu kutokuwa na hofu kwani serikali imeweka mikakati kuhakikisha watu wote wanakuwa salama.