Katibu Mkuu wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), John Mnyika amezungumzia tetesi zinazoendelea kwenye mitandao ya kijamii kuwa mwaka huu chama hicho kimepanga kumsimamisha aliyekuwa Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu kugombea nafasi ya Urais.
Akizungumza kwenye mahojiano maalum na kituo cha Television cha ITV, Mnyika aliulizwa kuhusu tetesi hizo, ambapo alieleza kuwa jukumu hilo ni la Kamati Kuu, na yeye ni sehemu tu ya mchakato huo.
“Mimi ni msimamizi wa uchaguzi na uchaguzi wa mgombea ni sehemu ya uchaguzi,” alisema Mnyika. “Naomba kwa sasa nisiseme chama kinamsimamisha nani kugombea nafasi ya urais 2020, Katiba yetu inasema Kamati Kuu ndiyo yenye mamlaka ya kutafiti jina la mgombea urais,” aliongeza.
“Lakini niwahakikishie Watanzania, Chadema itasimamisha mgombea wa urais ambaye ana uwezo wa kushinda na kuleta mabadiliko ya kweli,” aliongeza.
Mwaka 2015, Chadema iliungana na vyama vingine vitatu vya upinzani kuunda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) ambapo walimsimamisha Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa kugombea nafasi ya Urais. Lowassa alijiunga na chama hicho akitokea Chama Cha Mapinduzi (CCM) baada ya chama hicho kutopitisha jina lake kwenye mchakato wa kumpata mgombea urais.
Lowassa alichuana na mgombea wa CCM, Dkt. John Magufuli; matokeo rasmi yalionesha Dkt. Magufuli alishinda na hatimaye aliapishwa kuwa Rais wa Awamu ya Tano wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Hata hivyo, Machi Mosi, 2019 Lowassa alitangaza kurejea tena CCM akitumia maneno machache, “nimerudi nyumbani.”