Waumini 20 wamekufa mkoani Moshi kwa kukanyagana wakiwa katika jitihada za kukanyaga mafuta ya upako kwenye kongamano la Mtume Boniface Mwamposa lililofanyika uwanja wa Majengo.

Tukio hilo limetokea jana jioni, Jumamosi Februari 1, 2020, huku taarifa zaidi zikieleza kuwa zaidi ya watu 40 walikanyagana katika harakati hizo na kukimbizwa katika hospitali ya Rufaa ya mkoa wa Kilimanjaro ya Mawenzi.

Bado kuna hofu ya kuongezeka kwa idadi ya vifo kwani bado hakuna taarifa kamili ya majeruhi ambao wamepelekwa katika vituo vya afya vya jirani pamoja na hospitali ya rufaa ya KMC.

Mkuu wa wilaya ya Moshi, Kippi Warioba amethibitisha tukio hilo alipoongea na gazeti la Mwananchi usiku wa jana na kusema kuwa kwa taarifa za awali waumini waliofariki ni 20 lakini bado idadi kamili haijapatikana.

“Taarifa za awali tulizonazo ni kuwa waumini 20 wamepoteza maisha lakini tunaendelea kufuatilia maeneo mengine ya zahanati, vituo vya Afya na hospitali kama kuna watu waliopelekwa huko”  amesema Kippi.

 

Maiti za Virusi vya Corona China kuchomwa moto
Mahakama yazuia wananchi kusajiliwa kwa alama za vidole