Mara baada ya Rais wa Marekani, Donald Trump kumaliza kusoma hotuba yake aliususia mkono aliopewa na Spika wa Bunge la Wawakilishi nchini Marekani, Nancy Pelosi, ambaye naye kwa kulipizia aliamua kuichana hotuba hiyo mbele yake.
Jambo hilo limetokea wakati Trump akitoa hotuba kuhusu hali ya uchumi wa nchi hiyo kwa majigambo akidai kuwa amefanikiwa kuukarabati uchumi wa Marekani na hadhi ya nchi hiyo, ambavyo amesema vilikuwa vimewekwa rehani na watangulizi wake.
”Miaka ya uozo wa kiuchumi imekwisha. Siku za Marekani kuhujumiwa kiuchumi na kukejliwa na mataifa mengine tumeziacha nyuma. Tumeipa pia kisogo mienendo ya kuvunja ahadi, na kutafuta visingizio vya kumomonyoka kwa uchumi, nguvu na fahari ya Marekani,” amesema Trump na kuongeza kuwa kwa miaka mitatu tu, ”tumevunjilia mbali mienendohiyo na mitazamo Marekani inadidimia.”
Pelosi alitaja sababu ya kuchana hotuba hiyo kwa kusema alijaribu kutafuta kitu chochote cha kweli na cha maana kwenye hotuba hiyo na hakukiona.
Tukio hilo ni mwendelezo wa mvutano kutaka Trump aondolewe madarakani.
Aidha, zoezi zima lilianza vibaya pale Rais Trump alipokataa kuupokea mkono alionyooshewa na spika wa baraza la wawakilishi, Bi Nancy Pelosi, na kuuacha ukining’inia hewani.
Hivyo ililazimika Pelosi kumjibu Trump kwa mtindo wa jino kwa jino, alipoichana vipande-vipande nakala ya hotuba ya Trump aliyokuwa amekabidhiwa, mara tu Trump alipomaliza kuzungumza.