Waziri wa zamani wa Mambo ya Nje, Bernard Membe ambaye leo asubuhi anatarajia kufika mbele ya Kamati ya Udhibiti na Maadili ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) kwa ajili ya kuhojiwa, amesema alikuwa anasubiri kwa hamu kikao hicho.
Mwanasiasa huyo ambaye Katibu Mkuu wa chama hicho, Dkt. Bashiru Ally aliwahi kushangazwa na kutoonekana kwake kwenye shughuli za kichama tangu mwaka 2015, amesema kuwa amejipanga kuwaeleza wanakamati wanayoyajua na wasiyoyajua, katika kikao kinachofanyika leo kuanzia saa tatu asubuhi jijini Dodoma.
“Ninawaambia Watanzania, kesho ni siku muhimu sana, nilikuwa ninasubiri sana kukutana na hii Kamati kwa sababu nitapata nafasi ya kuzungumza na wanakamati mambo wasiyoyajua na wanayoyajua,” Membe alifunguka kwenye Mahojiano yake na AZAM TV, jana, Februari 5, 2020.
Alisema kuwa anaamini uamuzi wa Kamati hiyo utawasilishwa kwenye Kamati Kuu ya chama ambayo inaweza kutoa majibu yake ndani ya kipindi cha mwezi mmoja, ili hatima ya yote ijulikane.
Aidha, Membe alipoulizwa kama atakubaliana na uamuzi wowote wa kamati, alijibu kwa ufupi, “inategemea.”
Ameeleza kuwa atazungumza na waandishi wa habari baada ya kumaliza kikao na Kamati hiyo kwakuwa mambo yote yalikuwa yanajulikana kwa umma hata kabla.
Membe ataungana na waliokuwa Makatibu Wakuu wa chama hicho, Abdulrahman Kinana na Yusuf Makamba watakaohojiwa leo.
Sakata lao lilipata moto zaidi baada ya kusambaa kwa sauti zao wakisikika wanazungumza kwa mtazamo hasi kuhusu mpasuko ndani ya chama hicho. Wengine ambao sauti zao zilisikika lakini waliomuomba msamaha Mwenyekiti wa chama hicho, Rais John Magufuli na wakasamehewa, ni pamoja na Mbunge wa Mtama, Nape Nnauye, Mbunge wa Bumbuli, Januari Makamba na Mbunge wa Sengerema, William Ngeleja.
-
Membe afunguka alivyokipania kikao cha Kamati ya CCM