Ripoti ya ujenzi ya The Africa Construction Trends Report (2019) iliyoandaliwa na Kampuni ya Deloitte kutoka Uingereza inaonesha Tanzania inaongoza Afrika Mashariki kwa kuwa na miradi mikubwa ya ujenzi.
Ripoti inaonyesha Tanzania na Kenya zote zilikuwa na jumla ya miradi 51 mwaka 2019, lakini miradi ya Tanzania pekee ina thamani ya dola bilioni 60.3 ambazo ni takriban Tsh. trilioni 139, huku miradi ya Kenya ikiwa na thamani ya dola bilioni 36 ambazo ni takriban Tsh. trilioni 83.2.
Kwa mujibu wa ripoti hiyo, kwa ujumla miradi yote katika nchi za Afrika Mashariki iliongezeka kwa asilimia 30.9 kati ya mwaka 2018 na mwaka 2019, ambapo miradi inayoendelea kutekelezwa ni 182.
Imeelezwa kuwa nchi za Afrika Mashariki zinajumuisha asilimia 40.3 ya miradi yote barani Afrika ambayo thamani yake ni sawa na asilimia 29.5 ya miradi inayotekelezwa Afrika
Kwa sasa serikali ya Tanzania inatekeleza miradi mikubwa ya kiuchumi ikiwa ni pamoja na mradi wa kufua umeme katika Mto Rufiji utakaozalisha megawati 2115.