Mwita Nyamahano (48) amefikishwa katika Mahakama ya mwanzo wilaya ya Bunda mkoani Mara kwa kutelekeza familia.
Nyamahano alikamatwa katika operesheni ya tokomeza ubadhirifu na ukatili Mihingo (OTUUMI) iliyoanzishwa na ofisa mtendaji wa kata hiyo, Kichwabuta Shaaban.
Katika operesheni hiyo iligundulika kwamba kuna mwanamke mmoja ana watoto sita wakiwemo pacha waliot na sasa watoto hao wanakabiliwa na ugonjwa wa nimonia na utapiamulo.
Kwa mujibu wa mke wake huyo, Rhobi Kerumbe (28) amesema mumewe baada ya kuitelekeza familia yake alimwambia kuwa hawezi kumpatia mahitaji yoyote kikiwemo chakula.
Watoto hao kwa sasa wamelazwa kwenye hospitali teule ya halmashauri ya mji wa Bunda, ambapo Muuguzi mkuu wa wodi ya watoto amesema kwa sasa afya zao zinaendelea vizuri na msaada ambao unahitajika ni wasamalia wema kuwapatia chakula, gharama za dawa pamoja na mavazi.
Mwanamke huyo aliyetelekezwa amewaambia waandishi wa habari kuwa aliolewa mwaka 2012 ” alitutelekeza mimi na watoto wangu wote sita bila kutupatia matumizi yoyote na nilipokuwa nikimwambia kuhusu chakula anasema eti nile watoto wangu”.
Mtoto wa kwanza ana miaka nane, wa pili mitano, wa tatu na wa nne ni mapacha wana miaka miwili na wa tano na sita ni mapacha pia wana miezi sita.