Waziri wa Afya, maendeleo ya jamii jinsia wazee na watoto, Ummy mwalimu ametoa wito kwa watanzania kuacha tabia ya kukumbatiana, kupeana mikono kipindi hiki cha mlipuko wa ugonjwa wa virusi vya Corona duniani japo bado haujaingia nchini.
Ameyasema hayo leo februali 29, 2020 alipoongea na waandishi wa habari jiji Dar es salaam jinsi Serikali ilivyojipanga kukabilina na virusi vya Corona na njia za kutumiwa na wananchi kujikinga na ugonjwa huo.
” Ninawashauri wananchi kujizuia kupeana mikono na kukumbatiana, hili linaweza kuwa gumu kwa watanzania lakini lazima niseme, lakini pia nawataka wananchi kuepuka kugusana na mtu mwenye dalili za magonjwa ya njia ya hewa hususani mwenye historia ya kusafiri maeneo au nchi zilizoathirika na ugonjwa huu” Amesema Ummy
Ameongelea kwa upande wa wafanyabiashara ambao wanatoa bidhaa zao nje ya nchi hasa ambazo zinamlipuko wa Corona, kubadilisha mfumo wa kuingiza bidhaa kwa kuanza kutumia njia ya mtandao.
“Tunatambua kwamba kuna watanzania wengi wanafanya biashara na nchi ambazo zina maambukizi ya ugonjwa huu, tunashauri wafanye biashara mtandao katika kipindi hiki cha mlipuko wa ugonjwa huu” Amesisitiza waziri Ummy.
Pia ametoa siku tatu kwa kila halmashauri hapa nchini kubainisha vituo ambavyo vimeandaliwa kwaajili ya wagonjwa watakobainika na virusi hivyo na kila mkoa kuhakikisha kwenye hospitali kuna eneo maalumu la kuwatenga watakao athirika.
Kwa upande wa watanzania waliopo China ambao ni 504 wakiwepo wanafunzi walio katika mji wa Wuhan ambapo ndio kitovu cha mlipuko, waziri amesema wapo salama hakuna muathirika.
Aidha amesema tokea januari 30 hadi februari 27, 2020 jumla ya wasafiri zidi ya elfu 11 wanaotokea kwenye nchi zenye maambukizi ikiwemo China wamefanyiwa uchunguzi ambao unahusisha kipimo cha ” scaning” ambacho kila anayepita uwanja wa ndege anakuwa tayari amepimwa.
Na amesisitiza kuwa vifaa vya kupimia vipo vya kutosha, dawa kwaajili ya wagonjwa zipo tayari na kitengo cha maabara ya taifa kilichopo NIMR kimeimarishwa kwa kuwekwa kipimo kinachotoa majibu ndani ya masaa manne hadi sita.