Tuzo ya Mo Ibrahim Foundation imekosa mshindi kwa miaka miwili mfululizo kati ya viongozi wa Afrika.

Rais wa zamani wa Liberia, Ellen Johnson Sirleaf alishinda tuzo hiyo mwaka 2017 lakini mwaka 2018 na mwaka jana hakuna kiongozi mstaafu aliyefanikiwa kutuzwa tuzo hiyo inayoambatana na kitita cha $5 milioni.

“Tuzo hii hutolewa kwa watu ambao wameongoza kwa ufanisi zaidi, kuleta amani, utulivu na maendeleo kwa watu wao. Kwa kuzingatia vigezo hivi, Kamati ya Tuzo hii imeshindwa kumpata mshindi kwa mwaka 2019,” alisema juzi Mwenyekiti wa kamati hiyo, Festus Mogae.

Aliongeza kuwa ingawa Afrika inakabiliwa na changamoto nyingi, wameona kuwa viongozi wake wengi [wastaafu] walishindwa kuzigeuza changamoto hizo kuwa fursa.

Hata hivyo, Mogae ameeleza kuwa wanaamini kuwa kutokana na juhudi za baadhi ya viongozi wa Afrika, kamati hiyo itafanikiwa kumpata mshindi wa tuzo hiyo hivi karibuni.

Tuzo hii hutolewa kwa viongozi wastaafu wa Afrika waliokuwa wamechaguliwa kupitia michakato ya kidemokrasia, ambao wameachia madaraka ndani ya kipindi cha miaka mitatu iliyopita, baada ya kukamilisha kipindi chao kwa mujibu wa katiba.

Uhakiki wa vyama vya siasa kuanza rasmi
Prof. Kabudi awasilisha ujumbe wa JPM kwa Trump