Imeelezwa kuwa unywaji wa pombe uliokithiri na matumizi mabaya ya dawa za macho ni chanzo kikubwa cha ugonjwa wa presha ya macho.
Hayo yamebainishwa jana, ikiwa dunia inaadhimisha siku ya presha ya macho, daktari bingwa wa magonjwa ya macho kutoka hospitali ya tafa Muhimbili -Mloganzila Catherine Makunda amesema ugonjwa huo unaendelea kuongezeka ambapo katika kliniki moja kwa wiki huona wagonjwa 20 hadi 25.
Sababu nyingine zilizo ainishwa ni zile za umri mkubwa kuanzia miaka 40, kurithi, uvutaji sigara uliokithiri na ugonjwa wa kisukari.
“Tunafanya upimaji wa shinikizo la macho kama sehemu ya kuadhimisha siku ya presha ya macho duniani, tunapima na wale wanaohitaji matibabu wanapewa dawa, tumeshapima wagonjwa 65 kati yao tisa wamekutwa na tatizo hilo” Amesema dkt.Makunda.
na kuongeza kuwa “Kwa umri tatizo linaanza ukiwa mzee ambapo chujio la maji linachoka, matumizi ya baadhi ya dawa za macho ambazo zilishakaa muda mrefu, nawashauri watu wasipende kwenda dukani kununua dawa bila kuwaona wataalamu”
Amesema pia wagonjwa wa presha ya jicho wanakumbana na unyanyapaa katika jamii zao hali inayosababisha kukata tamaa ya matibabu.
Aidha amesema tatizo la presha ya macho kwa watoto linasababishwa na maumbile ya kuzaliwa ingawa idadi yao ni ndogo.