Daraja la mto wa Simiyu lililopo barabara kuu ya Mwanza kwenda Musoma limefungwa kwa siku 10 ili kupisha matengenezo makubwa baada ya kuharibika kutokana na uchakavu, jambo lililosababisha vyuma kukatika.
Akiwasilisha taarifa ya ufungwaji wa daraja hilo, Meneja wa wakala wa barabara Tanzania (TANROADS) mkoa wa Mwanza, Mhandisi Marwa Rubirya amesema wamefunga barabara hiyo kuanzia machi 8 hadi 18 mwaka huu ili kupisha matengenezo makubwa ya daraja.
Ameongeza kuwa wameamua kufanya matengenezo ya haraka ili kujiepusha na hatari zitakazoweza kujitokeza kwani kuchelewa kwa ujenzi huo yaweza kuwa hatarishi kwa watumiaji wa barabara.
Akizungumza wakati wa ukaguzi wa daraja hilo mkuu wa mkoa wa Mwanza, John Mongella amesema kutokana na changamoto hiyo, njia zitafungwa kwa muda uliopangwa (saa 3 usiku hadi saa 11 aubuhi), kwa siku kumi ili kupisha matengenezo.
Asema Serikali ina mpango wa kujenga daraja jipya, hivyo hatua zinazofanyika sasa ni za muda mfupi, ambapo amewataka wananchi kuwa wavumilivu waweze kuboreshewa njia itakayo wanufaisha na kuendeleza ujenzi wa taifa.
Daraja hilo lilijengwa mwaka 1962, limeanza kuonesha nyufa baada ya vyuma vilivyokuwa vinalishikilia kukatika, baadhi ya wakazi wanaolitumia wameishukuru Serikali kwa kuliona tatizo hilo kabla maafa hayajatokea.