Mfungaji wa bao pekee la Young Africans katika mchezo dhidi ya Simba SC Bernard Morrison, amewashukuru mashabiki wa klabu hiyo, kwa kusema walitimiza wajibu wao wa kufika uwanjani, na kuishangilia timu yao bila kuchoka.

Morrison anaecheza nafasi ya kiungo mshambuliaji, aliwainua mashabiki wa Young Africans katika dakika 44, kwa kupiga mpira wa adhabu uliokwenda moja kwa moja wavuni na kuamsha shangwe kwa mashabiki wa klabu hiyo yenye maskani yake katika makutano ya mitaa ya Twiga na Jangwani jijini Dar es salaam.

Amesema kuwa alichokifanya dhidi ya Simba jana jumapili ni sehemu ya kitu anachokipenda na imetokana na ushirikiano kutoka kwa mashabiki waliojitokeza kwa wingi uwanjani.

“Nafurahi kufanya kile ambacho ninakipenda, kwani tulijiandaa vizuri na kila mchezaji alikuwa tayari kuona tunashinda na hicho ndicho kilitokea, shukrani kwa mashabiki kwa ushirikiano waliotuonyesha sisi wachezaji.”

Kuhusu mbinu alizozifikiria kabla ya kumtungua Aishi Manula kwa bao la mpira wa adhabu uliozama wavuni kufuatia kuchezewa rafu na Jonas Mkude nje kidogo ya 18, mshambuliaji huyo raia wa Ghana, amesema alitafakari kwa kina na kutumia ujuzi wa kupitisha mpira juu ya wachezaji wa Simba waliokua wamejipanga (Ukuta), na alifanikiwa.

“Nilitumia ujuzi mkubwa kufanya vile ilivyoonekana, nilijaribu kuupitisha mpira juu ya ukuta wa wachezaji wa Simba, na nilifanikiwa kuupeleka mpira moja kwa moja wavuni, kwa kweli nimefurahishwa sana na hatua hii ya kuifunga timu iliyosumbua kwa miaka minne dhidi yetu.”

Katika mchezo wa mzunguuko wa kwanza uliochezwa Januari 04/2020, mshambuliaji huyo aliyesajiliwa wakati wa dirisha dogo la usajili akitokea Aftika kusini, hakuwepo kutokana na taratibu za usajili wake zilikua hazijakamilishwa.

Morrison mwenye miaka 26 alitua Young Africans kama mchezaji huru, baada ya kusitishiwa mkataba wake ndani ya klabu ya Orlando Pirates ya nchini Afrika ya kusini.

Alikuwa mchezaji pekee kusajiliwa baada ya kuwasili kwa kocha Luc Eymael, huku historia ikionyesha amewahi kuchez akatika klabu za DC Motema Pembe DRC (2018), Orlando Pirates (2016-2018), AS Vita DRC (2015-2016), Ashanti Gold FC Ghana (2013-2015) na Hearts of Lions (2010-2013).

Waziri mkuu Sudan anusurika kuuawa
Corona Italia: Makanisa yasitisha ibada, papa asalisha kwa mtandao