Kocha wa mabingwa wa soka nchini Simba SC, Mbelgiji Sven Vandenbroeck amechaguliwa kuwa Kocha Bora wa mwezi Februari wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara msimu wa 2019 – 2020.

Vandenbroeck alirithi mikoba ya Mbelgiji mwenzake, Patrick Aussems ametwaa tuzo hiyo baada ya kuwashinda Mrundi Hitimana Thierry wa Namungo FC ya mkoani Lindi na Abdul Mingange wa Ndanda SC ya Mtwara.

Aidha mshambuliaji wa Ndanda FC Vitalis Mayanga amechaguliwa kuwa Mchezaji Bora wa mwezi Februari wa Ligi Kuu baada ya kuwashinda Reliants Lusajo na Blaize Bigirimana wote wa Namungo alioingia nao fainali.

Mwezi Februari, Simba SC imecheza mechi saba, imeshinda sita 2-0 dhidi ya Coastal Union, 2-1 dhidi ya Polisi Tanzania 3-0 dhidi ya Mtibwa Sugar, 1-0 dhidi ya Lipuli FC, 1-0 dhidi ya Kagera Sugar na 3-1 dhidi ya Biashara United na kufungwa moja dhidi ya JKT Tanzania 1-0.

Mabingwa hao watetezi, Simba SC wanaendelea kuongoza Ligi Kuu, wakiwa na pointi 68, wakifuatiwa na Azam FC yenye pointi 51 baada ya wote kucheza mechi 27, wakati Yanga ni ya tatu kwa pointi zake 50 za mechi 25.

Chama amuomba radhi Fei Toto
Mikutano ya SADC ana kwa ana yasitishwa