Rais wa Marekani, Donald Trump ametangaza hali ya dharura ya kitaifa kutokana na kuendelea kusambaa kwa virusi vya corona.
Trump amesema kuwa Serikali yake itafanya kila liwezekanalo kuhakikisha hali iliyopo inadhibitiwa na usalama wa afya za wananchi wake unarejea.
Akiwa na Makamu wa Rais, Mike Pence na viongozi wengine wa masuala ya afya alipozungumza na vyombo vya habari Ikulu, Machi 13, 2020, Trump alisema kuwa anatenga $50 bilioni kwa ajili ya kusaidia kupambana na virusi hivyo.
Kampuni ya Google pia imeunga mkono juhudi za kupambana na virusi hivyo. Kampuni hiyo imeweka zaidi ya wafanyakazi 1000 watakaokuwa wanasaidia kupitia mtandao huo kuhakikisha unatoa maelekezo ya sehemu ambazo kuna vituo maalum vya huduma ya afya inayohusu virusi vya corona.
Watu 1,701 wamethibitika kuathirika na virusi vya corona (Covid-19), na watu 40 wameshapoteza maisha nchini Marekani.
Serikali imechukua hatua za dharura ikiwa ni pamoja na kupiga marufuku mikusanyiko mikubwa, matukio ya michezo na katika majimbo kadhaa shule zimefungwa.