Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Constantine Kanyasu amekiagiza Kikosi Dhidi ya Ujangili ( KDU) Kanda ya Kaskazini kuongeza mbinu katika kukabiliana na ujangili wa wanyamapori wadogo wadogo wanaouawa kwa ajili ya kitoweo na baadhi ya wananchi wanaoishi maeneo yaliyo karibu na Hifadhi.
Ametoa agizo hilo leo mkoani Arusha wakati alipokuwa akizungumza na Watumishi wa kikosi hicho kinachokabiliana na na ujangili katika mikoa ya Arusha, Tanga, Kilimanjaro na Manyara.
Hatua hiyo inakuja kufuatia nguvu kubwa na mashirika ya Kiuhifadhi ya ndani na nje ya nchi kujielekeza katika ulinzi wa wanyamapori wakubwa kama vile tembo, faru, twiga, simba pamoja chui huku wanyamapori wadogo wakiwindwa kwa kasi na jamii zinazopakana na hifadhi kwa ajili ya kitoweo.
Akizungumza katika mkutano huo, Kanyasu amesema endapo hatua za makusudi hazitachukuliwa kukabiliana na tatizo hilo jamii nzima itakuwa hatarini wanyamapori kama vile Simba wataanza kuwala binadamu kwa vile wanyama wanaotegemewa kama chakula chao watakuwa wamekwisha kwa ujangili.
Amewataja wanyamapori hao wadogo wanaowindwa ni kama vile swala, pundamilia, sungura, nguruwepori pamoja na digidigi
Mbali ya athari hiyo, ametaja athari zingine ikwemo wanyamapori wakubwa watatoweka kwa kukosa chakula na hivyo sekta ya utalii itaathirika kwa vile kutakuwa na hifadhi zisizo na wanyamapori.