Klabu ya Ajax ya Nchini Uholanzi imevunja mkataba na kiungo Abdelhak Nouri baada ya mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 22 kuzinduka kutoka kwenye Coma siku chache zilizopita.
Nouri alipoteza fahamu kwa muda wa takribani miaka 2 na miezi 8 baada kuanguka na kupoteza fahamu katika mchezo kirafiki dhidi ya Werder Bremen ya Nchini Ujerumani Julai 8, 2017 Nchini Austria kutokana na shambulio la Moyo.
Kwa sasa Mouri anaweza kukaa kwenye kiti cha Magurudumu, kuzungusha macho pamoja na kula ambapo mpaka sasa Ajax wapo kwenye mazungumzo na Familia ya mchezaji huyo kwa ajili ya kujadili mustakabali wa maisha yake ya baadae.
Kaka yake ambaye anamhudumia wakati wote nyumbani, amesema, “hakuwepo nyumbani kwa muda mrefu, tunaangalia kwa ukaribu afya yake hapa. Hivi sasa anaweza kukaa, anafahamu kuwa yupo mahali gani, analala, anakohoa na anakula pia, bado anaendelea kuimarika akiwa anatutegemea.”
Abdelhak amecheza jumla ya michezo tisa akiwa na kikosi cha kwanza cha Ajax kabla ya kipaji chake kukatishwa katika tukio hilo.