Taasisi tatu zinazoaminika kuongoza kwenye tafiti za madawa na tiba, zimeungana kutafuta tiba au chanjo dhidi ya virusi vipya vya corona (Covid-19), ambapo jana wametangaza kupokea $20 Milioni kwa ajili ya kuwezesha utafiti huo.
Taasisi hizo za Marekani ni Chuo Kikuu cha Washington, Chuo Kikuu cha Oxford na Chuo cha Tiba cha La Jolla (La Jolla Institute for Immunology).
Uwezeshaji huo unatajwa kuwa mkubwa kutoka kwa wadau walioungana kupambana na Covid-19, ikifuatia muunganiko wa Taasisi ya Bill and Melinda Gates, Wellcome na taasisi ya Mastercard ambazo zote zina lengo la kusaidia kuharakisha upatikanaji wa chanjo na tiba ya virusi hivyo.
“Ruzuku hizi kwa taasisi zinazoongoza kwa tafiti za tiba itaongeza uelewa wetu kuhusu kiasi gani dawa tulizonazo sasa zinaweza kusaidia kupambana na virusi hivi vinvyoikumba dunia yote,” alisema Mark Suzman ambaye ni Ofisa Mtendaji Mkuu wa Bill and Melinda Gates.
“Uwekezaji huu wa awali kwenye Covid-19 itaongeza wigo wa kupata suluhusisho, hatua zaidi zitatangazwa na wataalam waliobobea kwenye tafiti na tiba,” aliongeza.
Aidha, yapo mashirika mengine ambayo yametangaza kuwekeza katika utafiti huo, ambapo taasisi ya Chan Zuckerberg imeahidi kuchangia $25 milioni na Serikali ya Uingereza imeahidi kutoa Euro 40 milioni.
Baadhi ya dawa ambazo zimewekwa maabara kwa ajili ya utafiti ni pamoja na chloroquine na hydroxychloroquine, ambazo bado hazijathibitishwa lakini zimewahi kutumika kutibu malaria kwa zaidi ya kipindi cha miaka 50.
Katika hatua nyingine, Shirika la Afya Duniani (WHO), limeziomba Jumuiya za Kimataifa kutoa $675 milioni kusaidia mataifa ambayo yana mifumo isiyo imara ya afya kama sehemu ya mpango mkakati wa kusaidia maandalizi na kujikinga na Covid-19.