Shirikisho la soka barani Ulaya UEFA, limetoa onyo onyo kwa nchi wanachama zinazohitimisha ligi zao mapema katika kipindi hiki cha janga la Corona, kwa kusema zinaweza kupoteza nafasi zao kwenye ushirikin wa michuano ya Ligi ya Mabingwa na Europa League msimu ujao.
Onyo hilo limetoka siku moja baada Ubelgiji kuhitimisha ligi yake kwa kuwatangaza Club Brugge kuwa mabingwa wa msimu huu licha ya kutomalizika kwa michezo yote ya ligi kuu.
Barua ya Uefa kwenda kwa bodi na vyama vya soka barani humo, imeeleza kuwa kuna mpango unaotengenezwa kwa ligi zote barani humo kumalizika mwezi Julai ama Agosti mwaka huu ikiwemo Ligi ya Mabingwa pamoja na Europa League ambazo ziko katika hatua ya 16 bora.
“Kwa kuwa kigezo kikubwa cha kushiriki michuano ya Uefa ni matokeo ya uwanjani baada ya ligi husika kukamilika kwa michezo yote kuchezwa, kuhitimisha ligi kabla ya wakati, kunaweza kuyafanya mataifa hayo kukosa sifa hiyo”, imeeleza barua hiyo.
Katika barua hiyo, Uefa imeeleza kuwa wana imani kuwa ligi zinaweza kurejea mwezi ujao, na michezo kuchezwa kwa masharti yatakayowekwa na mamlaka husika, na baada ya mabingwa kupatikana, ndipo msimu mpya wa ligi ya mabingwa utaanza.