Leo ni siku maalum inayotokea mara moja tu kwa mwaka, siku ambayo Wakristo karibu wote Duniani kote wanakumbuka kufufuka kwa Bwana Yesu Kristo. Ingawa siku hii huwa haina tarehe maalum, hufanyika Jumapili ya mwisho wa mwezi Machi au Aprili baada ya siku 30 za mfungo wa toba (kwarezima), lakini mbali na kumbukizi ya kiimani, wakati mwingine huja na matukio makubwa yanayoandika historia nzito.
Baadhi ya matukio ya kihistoria yaliyowahi kutokea Jumapili ya Pasaka ni ya kisiasa, kijeshi, Kisayansi na burudani yaliyogusa kiwanda cha burudani. Baadhi ya matukio hayo ni yafuatayo:
Ugunduzi wa Kisiwa cha Pasaka (Easter Island) – Aprili 5, 1722
Aprili 5, 1722, ilikuwa Jumapili ya Pasaka, mfanyabiashara Mholanzi, Jacob Roggeveen akiwa kwenye mizunguko yake duniani, katika eneo la Bahari ya Pacific, aligundua kuwepo kwa kisiwa cha aina yake kinachotokana na milipuko ya volcano.
Aliamua kukiita kisiwa hicho Paasch-Eiland, kwa lugha ya kwao, ikimaanisha ‘Easter Island’ kwa Kiingereza na ‘Kisiwa cha Pasaka’ kwa lugha adhimu ya Kiswahili. Kisiwa hicho ni maarufu kutokana na jinsi kilivyopambwa na sanamu za binadamu warefu ambao wanawakilisha binadamu wa zamani walioishi katika eneo hilo ambao walikuwa na urefu wa aina yake.
Mwaka 1995, UNESCO ilikiweka kisiwa hicho kwenye orodha ya maeneo ya aina yake ambayo ni Urithi wa Dunia. Kisiwa hicho kiko chini ya utawala wa Chile kikiwa umbali wa kilometa 3,600 tu kutoka katika mipaka ya Chile. Kisiwa hicho pia kinafahamika kwa jina la Rapa Nui.
Jiji la Tel Aviv, Israel liliasisiwa (Aprili 11, 1909)
kundi la wanafamilia wenye uchumi wa kati, walinunua ardhi Kaskazini-Mashariki mwa Jaffa, jiji ambalo ni bandari ya kihistoria. Waligawa ardhi hiyo katika viwanja (plots) 66 na wakagawana kwa mnada Aprili 11, 1909, Jumapili ya Pasaka.
Mwaka mmoja baadaye waliubatiza mji huo jina la Tel Aviv, Jina la Kiyahudi ambalo maana yake ni ‘mlima wa chemchem’. Hivi sasa Tel Aviv ni jiji la pili maarufu zaidi nchini Israel baada ya Jerusalem. Tel Aviv imekuwa kitovu cha Sanaa na maonesho na kisima cha uchumi wa Israel.
Sio hivyo tu, Tel Aviv ndio jiji ambalo linatembelewa zaidi katika eneo lote la Mashariki ya Kati.
Vita Kuu ya Pili ya Dunia, Mapigano ya Okinawa (April 1, 1945)
Aprili 1, 1945 ilikuwa Jumapili ya Pasaka, Jeshi la Marekani na washirika wake lilivamia eneo la Japan na kuanzisha mapigano makali yaliyolenga kuteka kisiwa cha Okinawa, ili wakitumie kama ngome yao ya kijeshi kuwasaidia kuishambulia vizuri Japan.
Mapigano hayo yanatajwa kuwa na madhara makubwa zaidi tangu vita hiyo ianze katika eneo hilo. Mapigano katika eneo hilo yalidumu kwa siku 82, kuanzia Aprili Mosi hadi Juni 22, 1945. Pia, yalibatizwa jina la ‘Typhoon of Steel’, yaani kimbunga cha chuma. Marekani walitumia kikosi maalum cha Makomando wake kilichoitwa ‘The Tenth Unit’, na Japan wao wakatumia kikosi chake cha maangamizi yaliyohusisha pia kujitoa mhanga kiitwacho ‘Kamikaze’.
Makumi elfu ya watu walipoteza maisha katika mapigano hayo. Inaelezwa kuwa kulikuwa na majeruhi zaidi ya 160,000 kwa ujumla kwa pande zote (Marekani na Japan, ingawa idadi ilikuwa kubwa kidogo kwa upande wa Japan. Wakaazi 149,425 wa Okinawa walipoteza maisha au kutojulikana walipo. Pande zote zilipoteza meli kubwa na ndege.
Agosti 6 na Agosti 9, 1945 Marekani kwa ruhusa ya Uingereza ilishusha mabomu ya atomic kwenye miji ya Nagasaki na Hiroshima ya Japan. Septemba 2, 1945 Japan ilikubali kushindwa na Vita Kuu ya Pili ya Dunia ikahitimishwa. Marekani ikachukua eneo la Kisiwa cha Ryukyu ambacho Okinawa ni sehemu ya kisiwa hicho. Ilikimiliki hadi mwaka 1972 ilipoirudishia tena Japan.
Georgia yapiga kura kujitenga na Urusi (Machi 31, 1991)
Georgia ilikuwa sehemu ya Umoja wa Kisoviet (USSR), lakini wanaharakati wa eneo hilo walihamasisha watu kupiga kura ya kujiondoa kwenye umoja huo. Machi 31, 1991 ikiwa ni Jumapili ya Pasaka, asilimia 90.6 ya raia wa Georgia walijitokeza kupiga kura.
Matokeo ya kura hizo yalikuwa ya kishindo kizito, ambapo asilimia 99.5 ya wapiga kura wote walichagua kujitenga. Baraza Kuu la Georgia lilipitisha uamuzi huo wa wananchi, Aprili 9. Lakini kutokana na kukamilisha taratibu, Georgia ilijitenga rasmi Desemba 26, 1991, siku ambayo USSR ilivunjwa rasmi na kuunda Urusi.
Captain Phillips aokolewa kutoka mikononi mwa Maharamia (Aprili 12, 2009)
Aprili 8, 2009 Meli ya Marekani, MV Maersk Alabama ilivamiwa na maharamia katika pwani ya Somalia, Mashariki mwa Afrika. Maharamia walimteka Captain Phillips na kumtumia kudai pesa kutoka Marekani.
Hata hivyo, Aprili 12, 2009 ikiwa ni Jumapili ya Pasaka, vikosi vya maji vya makomando wa Marekani vilifanikiwa kumuokoa Captain Phillips.
Hatua hiyo ilikuwa ushindi uliobadili hali ya hewa na kuongeza nguvu ya kupambana na maharamia katika pwani hiyo. Sasa yamekomeshwa kwa kiasi kikubwa.
Mwaka 2013, simulizi la mkasa huo liliwekwa kwenye filamu iliyoitwa ‘Captain Philips’, mhusika mkuu akiwa Tom Hanks, na ilitumia raia wa Somalia.
Kutolewa tuzo za ‘The Tony’ kwa mara ya kwanza (Aprili 6, 1947)
Kwa mara ya kwanza Tuzo zinazoheshimiwa sana nchini Marekani kwenye sanaa ya maigizo na maonesho ya jukwaani ‘The Tony Awards’ zilitolewa Jumapili ya Pasaka, Aprili 6, 1947 jijini New York.
Hadi sasa imesafanyika zaidi ya mara 70 ikiwa na vipengele 26.
Kumbukizi za siku ya kuzaliwa:
Lakini kwa kuongezea tu, Aprili 19, 1987 ikiwa ni siku ya Jumapili ya Pasaka, nchini Urusi alizaliwa Maria Sharapova, mchezaji wa tennis maarufu mwenye mafanikio makubwa. Na Machi 30, 1986 alizaliwa Kapteni wa timu ya Real Madrid na Timu ya Taifa ya Hispania, Sergio Ramos.
Endelea kusherehekea mapumziko ya Pasaka, lakini hakikisha unazingatia maelekezo ya Serikali ili kuepuka maambukizi ya virusi vya corona. Hakikisha matukio yanayotokea leo yanakuwa ya furaha, amani na kuifanya dunia kuwa sehemu nzuri zaidi ya kuishi.