Serikali imesema wataalamu wa afya, wanafanya mchakato wa namna bora na sahihi ya jinsi ya kutengeneza barakoa zinazofaa kuvaliwa kwa wananchi kama njia mojawapo ya kujikinga na Corona.
Naibu Waziri wa Afya, Dkt. Faustine Ndugulile amesema wataalamu watakapokamilisha mchakato huo, Wizara itatoa maelekezo kwa wananchi ya jinsi ya kuzitengeneza barakoa hizo.
Amesema barakoa zinazotengenezwa kwa vitambaa vya nguo, ndizo zitatolewa maelekezo ya namna ya kuzitengeneza, ili wananchi waweze kuzitumia kupunguza kasi ya maambukizi ya Covid 19 na kufuata maelekezo mengine ya jinsi ya kujikinga.
Dkt. Ndugulile amesema N 95 ni aina ya barakoa kwa wakati zinapaswa zitumike zaidi na wanaohudumia wagonjwa wa Covid 19 moja kwa moja, kwa sababu kidunia uzalishaji wake umepungua.